Mpachika mabao wa Yanga, Amissi Tambwe, amewaambia viongozi wa timu hiyo kama wanataka kuona makali zaidi ndani ya uwanja, basi wamsajili Mrundi mwenzake, Didier Kavumbagu anayekipiga Azam FC.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kupata taarifa za mshambuliaji huyo kuwa yupo tayari kurejea kuitumikia Yanga katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara mara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kavumbagu aliondoka Yanga msimu uliopita baada ya mkataba wake kumalizika kabla ya Azam FC kumsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao unaelekea ukingoni, hivyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomhitaji.
Tambwe amesema kuwa kama timu yao ikifanikiwa kumsajili Kavumbagu, basi kikosi chao kitatisha katika safu ya ushambuliaji kutokana na uwezo mkubwa wa mshambuliaji huyo.
“Hivi ni kweli hizo taarifa kwamba Kavumbagu anataka kurudi Yanga? Kama ni kweli taarifa hizo basi Yanga imsajili haraka kwa ajili ya kuiboresha safu yetu ya ushambuliaji, ukiangalia hivi sasa anaongoza kwenye ufungaji akiwa na mabao 9, ni mshambuliaji anayetakiwa kuichezea Yanga.
“Ninaujua vizuri uwezo wa Kavumbagu, ni mchezaji tunayecheza naye wote timu ya taifa ya Burundi, ninaamini kabisa akitua kuichezea Yanga, basi timu yetu itakuwa bora zaidi kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao,” alisema Tambwe huku akicheka.
Kavumbagu amekuwa gumzo kubwa hivi sasa katika soka la Bongo, kutokana na uwezo wake mkubwa anaouonyesha katika kuzifumania nyavu akiwa na Azam FC.