MABINGWA wa zamani wa ligi kuu bara Yanga SC jioni ya leo katika uwanja wa Taifa inatarajia kupambana vikali na timu ya Kagera Sugar ya mjini Bukoba mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara mchezo wa marudiano.
Yanga ambayo ina kumbukumbu ya kufungwa 1-0 na timu hiyo zilipokutana katika raundi ya kwanza kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba leo itataka kulipiza kisasi, pia haitakubali kupoteza mchezo huo hasa ikizingatiwa kipindi hiki ni cha ushindani mkubwa.
Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 31 huku wapinzani wao katika mbio za ubingwa Azam FC yenyewe ina pointi 33, hivyo Yanga itataka kushinda mchezo huo ili iweze kukalia usukani, pia hasimu wake mkuu Simba ambaye naye anajitupa uwanjani jijini Tanga dhidi ya Mgambo JKT.
Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29 hivyo inawapa wakati mgumu Yanga na kuifanya ishinde mchezo wa leo, endapo Yanga itashinda mchezo huo itakamata nafasi ya kwanza huku vita hiyo ya kukimbizana ikizidi kuwa kubwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Yanga ilitoa dozi nzito kwa timu ya FC Platinum ya Zimbabwe mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika Yanga ilishinda mabao 5-1 hivyo ushindi huo unawapa hamasa kubwa katika mchezo wao wa leo huku ikijivunia safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Mrundi Amissi Tambwe na Mrisho Ngasa