come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

CHEKA ATOKA JELA

Bondia maarufu nchini, Francis Cheka (pichani), aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kumpiga meneja wake, amepunguziwa adhabu na sasa atatumikia kifungo cha mwaka mmoja akiwa uraiani.

Ofisa Ustawi wa Jamii, Yusufu Fonera, alisema jana kuwa Cheka ametoka gerezani kwa mujibu wa Sheria ya Magereza Namba 34 ya mwaka 1967 kifungu cha 51 kilichofanyiwa marekebisho ya sheria namba 9 mwaka 2002 kinachompa uwezo mkuu wa gereza kuomba kupunguzwa kwa adhabu ya mfungwa.

Alisema kifungu hicho cha sheria kinamruhushu mkuu wa gereza kuiomba ofisi ya ustawi wa jamii kubadilisha au kupunguza adhabu kwa mfungwa endapo tu itaridhika na tabia ya mfungwa huyo akiwa gerezani.


Fonera alisema kuwa baada ya ustawi wa jamii kupokea ombi hilo huitaarifu mahakama (hasa mahakama iliyotoa hukumu) ambayo hutoa mabadiliko ya hukumu na mfungwa kuanza kutumikia adhabu mpya ambayo inaweza kuwa ni kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii kama ilivyofanyika kwa Cheka.

Alisema kutokana na mwenendo wa tabia ya Cheka gerezani, bondia huyo aliyepata kutwaa taji la dunia, amebadilishiwa adhabu na kuanza kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii kama kufagia, kufyeka tangu jana.

Alisema, Cheka ni miongoni mwa watu 50 walioombewa na mkuu wa gereza kupunguziwa adhabu baada ya kuonyesha tabia nzuri ya uadilifu gerezani.

Cheka ataendelea kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii hadi Februari mosi, 2017 atakapokuwa huru na kwamba katika kipindi hiki Cheka hatakiwi kufanya uhalifu wowote wala kutoka nje ya mkoa wa Morogoro bila taarifa.

Awali, Februari 2, mwaka huu, Cheka alihukumiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Said Msuya kwenda jela na kulipa faini ya Sh. milioni 1 mara atakapotoka gerezani kwa kosa la kujeruhi mwili.

Alitenda kosa hilo kwa kumpiga Bahati Kibanda aliyekuwa meneja wa baa yake.