Mshambuliaji wa Yanga, Hussein Javu, ameweka wazi kuwa kinachomfanya asing’ae na asirudi kwenye makali yake kama ilivyo zamani ni muda mdogo anaoupata katika kuitumikia timu hiyo kwenye mechi zake za ligi na michuano ya kimataifa.
Javu ambaye alisajiliwa Yanga msimu wa 2012/13 akitokea Mtibwa Sugar baada ya Yanga kushawishika na kazi yake aliyokuwa akiifanya Mtibwa kwa sasa, amekosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akipata ushindani mkubwa wa namba kutoka kwa mastraika wengine wa timu hiyo.
Javu alisema kwamba anaamini kuwa bado ana uwezo mzuri isipokuwa kutokucheza mara kwa mara, kuna kitu huwa kinapungua katika ufanisi wake, hivyo anaamini kama atakuwa anatumika mara nyingi zaidi katika timu hiyo basi atarejea kwenye makali yake kama ilivyokuwa awali.
“Bado ninaamini kuwa nina uwezo mzuri na naweza kucheza zaidi lakini kwa upande wangu naona kama muda wa kutocheza mara kwa mara au kutotumika kwa muda mwingi ndani ya timu ndiyo linakuwa tatizo kubwa.”