SAFU ya ushambuliaji ya Yanga kwa sasa ina mapungufu makubwa, yamejitokeza kwenye mechi zake za mwanzo na kupelekea baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuanza kuwakumbuka nyota wao waliokosekana katika mechi hizo.
Yanga ina pengo kubwa hasa la Mrisho Ngasa (Pichani) ambaye yuko kifungoni, hilo ni jambo la kushangaa tena sana, unaweza ukakosa fedha lakini ukawa na uzima wa afya huku ukijipa matumaini kwamba kesho utapata.
Lakini Yanga imekosa kila kitu kwa sasa, hakuna tena furaha baada ya kukosekana kwa huduma ya Mrisho Ngasa (Pichani), nikiwa zatazama mechi moja mchangani mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Yanga ikicheza na Mbeya City jijini Mbeya, rafiki yangu mmoja alisema kwamba Yanga itashindwa kuibuka na ushindi na kucheza kandanda safi kwa sababu haina Ngasa.
Ngasa ni mchezaji mahiri kabisa ambaye kukosekana kwake kutaiathili Yanga msimu huu, maneno yake yakaja kutimia baada ya mchezo huo kumalizika na matokeo ikiwa Yanga 1 Mbeya City 1.
Yanga iliponea tundu la sindano na kama si jitihada binafsi zilizofanywa na Kavumbagu huenda kikosi hicho kingelala, Uwepo wa Ngasa unaweza kuwainua Didier Kavumbagu na Jerry Tegete ambao wanaonekana bado hawajapata mtu wa kuwalisha mipira.
Kavumbagu ni straika makini awapo karibu na lango lakini anajikuta anashindwa kupachika magoli kutokana na kutopewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viungo wachezeshaji.
Lakini Ngasa anatajwa kama miongoni mwa viungo bora kabisa wanaong'ara kwa utoaji pasi za mafanikio, msimu uliopita Ngasa alitoa pasi 25 zilizozaa magoli alipokuwa Simba SC.
Hadi sasa uongozi wa Simba unahaha na kudai TFF imewafanyia hujuma kumkosa Ngasa, waliamini kuwa ndiyo suluhisho lao la magoli, ila msimu huu Ngasa anaitumikia Yanga lakini mpaka sasa bado hajaanza kuichezea kutokana na adhabu aliyopewa na TFF.
ALIPOTOKEA NGASA
Mrisho Ngasa ni zao la Toto Afrika ya Mwanza ambapo alianza kuichezea akiwa na umri wa miaka 14, jitihada zake zilimwezesha kuitwa timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys iliyoshiriki kwa mafanikio fainali za kombe la mataifa Afrika mwaka 2002.
Kikosi hicho cha Serengeti kilifikia mafanikio hayo kikiwa chini ya kocha mzalendo Abdallah Kibaden, lakini ikajikuta inaondoshwa mashindanoni baada ya kumtumia mchezaji aliyepita umri.
Kilikuwa kikosi bora kabisa kuwahi kutokea hasa kwa timu za taifa za vijana hapa nchini, ilikusanya nyota ambao leo hii tegemeo la taifa, Ngasa alikuwa miongoni mwa wachezaji waliong'ara katika timu hiyo wakiwemo Athuman Idd 'Chuji', Nizar Khalfan, Nurdin Bakari, Amir Maftah, Julius Mrope na wengineo.
Baadaye Ngasa alisajiliwa na Kagera Sugar na alikuiwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha timu hiyo kutwaa kombe la Tusker baada ya kuilaza Simba mabao 2-0 yaliyofungwa na Omari Changa.
Ngasa aliitwa timu ya taifa ya wakubwa iliyokuwa ikinolewa na Mbrazil Marcio Maximo ambayo nayo iliweka rekodi ya kufuzu fainali za kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN.
Ngasa alisajiliwa na Yanga na hapo ndipo alipoweza kutangaza jina, alipata ofa mbalimbali za kutakiwa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ambapo hadi sasa ameweza kuweka historia kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mechi ya pamoja na Manchester United.
Ngasa alipata nafasi ya kucheza na Rio Ferdinand, Wayne Rooney, Michael Carrick na wengineo kitu ambacho ni kigeni kwa wachezaji wa Kitanzania.
Ngasa alipata nafasi hiyo alipokwenda kufanya majaribio katika klabu ya Seatle Sounders ya Marekani, Azam ilimchukua Ngasa akitokea Yanga kisha kumpeleka kwa mkopo Simba.
Kuna mengi ameyafanya Ngasa akiwa Azam na Simba, Wanayanga wataanza kupata huduma ya Ngasa mara baada ya kumaliza adhabu yake ya kusajili timu mbili kama alivyoadhibiwa na TFF, Sitaki kueleza kiundani kuhusu adhabu hiyo lakini ukweli wa yote anayo Ngasa mwenyewe.
USICHOKIJUA KUHUSU NGASA
Ngasa alizaliwa mwaka 1989 mkoani Kagera ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza (TP Lindanda wana kawekamo) na Taifa Stars mzee Khalfan Ngasa 'Babu'.
Mama yake mzazi Ngasa ni mhaya wa Bukoba wakati baba yake ni msukuma mwenyeji wa Mwanza, ila alilelewa kwa mama Bukoba, anatajwa kama mchezaji pekee mwenye kumiliki nyumba ya kifahari kuliko mchezaji yeyote nchini.
Pia anamiliki magari ya thamani na hivi karibuni alinunua gari lingine la wazi ambalo linasemekana ni bei mbaya, huyo ndiye Mrisho Ngasa ambaye anasubiriwa kwa hamu kubwa kuitumikia Yanga kwa mafanikio, je atang'ara ni suala la kusubiri kisha tuone.