Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wamewataka mashabiki wa klabu hiyo kutovunjika moyo na timu yao kutokana na matokeo ya sare tatu mfululizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini hapa, wachezaji hao wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo, walisema matokeo waliyoyapata katika michezo dhidi ya Coastal Union, Mbeya City na Prisons si mazuri, lakini lazima wakubali kwamba soka ndivyo lilivyo.
“Matokeo si mazuri sana… lakini ndivyo soka lilivyo, huwezi kushinda kila mchezo..., mashabiki wasikate tamaa ligi ndiyo kwanza imeanza, cha muhimu ni kujipanga upya na kuangalia michezo inayofuata,” alisema Niyonzima.
Canavaro kwa upande wake aliwataka mashabiki kundelea kuwasapoti kwa sababu bado imebaki michezo mingi kwenye ligi hiyo.
“Bado kuna michezo mingi mbele yetu, tumeteleza kwa kutoka sare michezo mitatu…, kwetu matokeo haya hayawezi kutukatisha tamaa, badala yake yanatuongezea morali ya kuhakikisha tunashinda michezo ijayo,” alisema Cannavaro.
Wachezaji hao walisema kuwa hawakucheza vizuri kwenye mchezo dhidi ya Prisons kwa kuwa walikosa umakini licha ya kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufungwa kwenye mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 kama ilivyokuwa ile ya Coastal na baadaye dhidi ya Mbeya City.
Yanga sasa inajiandaa kuvaana na Azam FC kwenye mchezo unaofuata wa ligi kuu utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.