come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA YANASA SIRI ZA ETOILE DU SAHEL, SASA WAMEKWISHA

Yanga imepata CD zinazoonyesha mechi kadhaa za hivi karibuni za wapinzani wao katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika, timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, imeelezwa.

Yanga na ESS zitacheza mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe la shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo na kurudiana wiki mbili baadaye Tunisia.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema uongozi umepata "mikanda ya video ya hivi karibuni ya Etoel du Sahel ambayo itamsaidia kocha (Hans van der) Pluijm" katika maandalizi.


Pluijm alithibitisha habari hizo kutoka kwa kiongozi ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa sababu si msemaji wa klabu kwa kuuambia mtandao huu kuwa ameanza kuwafuatilia wapinzani wao hao kwa kuangalia michezo yao ya hivi karibuni.

Mholanzi huyo ambaye aliiwezesha Berekum Chelsea ya Ghana kucheza robo-fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2012, alisema anaifuatilia kwa karibu Etoile kwa sababu anajua kuwa ni moja ya vigogo vya soka barani.

Pluijm alisema kuwa tayari ameshaanza mikakati na mipango ya kukabiliana na kuwashinda waarabu hao kwenye uwanja wa nyumbani.

"Nafahamu Etoel ni timu kubwa kimafanikio Afrika ukilinganisha na timu yangu lakini siwahofii kwa sababu naamini nina kikosi kizuri na ninataka kumaliza kazi kwenye uwanja wa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana nao kwao," alisema Pluijm.

Alisema kuwa mchezo huo wa Jumamosi umekuja wakati sahihi ili kuthibitisha ubora na uimara wa Yanga ambayo imefika hatua hiyo baada ya kuzitoa timu za BDF XI ya Botswana na Platinum ya Zimbabwe.

"Tunakabiliwa na mchezo wa ligi Jumapili (kesho) lakini nimeshaanza mikakati na programu dhidi ya Etoel na kwa kweli nawashukuru viongozi wa Yanga kwa ushirikiano wanaonipa kuelekea kwenye mchezo.

"Mimi nasema wana Yanga na Watanzania wote watulie kwa sababu tumejipanga kuhakikisha tunaingia hatua ya kumi na sita bora na tutamaliza kazi hapa nyumbani," aliongezea kusema Pluijm.

Yanga ilianza kwa kuifunga BDF IX 3-0 lakini ikachapwa 2-1 ugenini kabla ya kuifunga Platinum 5-1 na kwenda kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa marudiano nchini Zimbabwe.

Mara ya mwisho Yanga kukutana na waarabu iliifunga Al Ahly ya Misri 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika chini ya Pluijm kwenye Uwanja wa Taifa mwaka jana lakini ikatolewa kwa matuta ugenini baada ya sare ya 1-1.