Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye
Tayari timu ya FC Lupopo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa imeandika barua ya kuomba kushiriki michuano hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dafur jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisema kuwa maandaalizi ya mashindano hayo yanaendelea vyema lakini akasema kwamba mwaka huu hakutakuwa na timu mwalikwa.
Musonye alisema kwamba klabu 13 kutoka kwa nchi wanachama wa CECAFA zitashiriki tofauti na miaka mingine ambapo timu zinazothibitisha na kufika kwenye michuano huwa 11 na shirikisho hutoa nafasi moja kwa timu nyingine kutoka nje ya ukanda kuchuana kuwania kitita cha Dola za Marekani 30,000 zinazotolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
"Timu zetu zitakuwa 13 hivyo tayari tutakuwa na mechi nyingi za kutosha kwa kila kundi kwenye mashindano haya, na sasa naongea nikiwa Dafur, maandalizi yako kwenye hatua za mwisho na hali ni salama," alisema Musonye ambaye ni raia wa Kenya.
Alitaja baadhi ya timu zinazotarajiwa kushiriki kuwa ni pamoja na mabingwa watetezi, Yanga, na Simba kutoka Tanzania Bara, KMKM ya Zanzibar na Tusker (Kenya) na APR ya Rwanda.
Musonye alisema kwamba wenyeji wa mashindano hayo watawakilishwa na klabu tatu ambazo ni El Mereikh, El Hilal na Al Ahly Shandy na tayari wameshaingia kambini wakijiandaa na michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.
Aliongeza kuwa mwana huu mashindano yanatarajiwa kuwa na ushindani kwa sababu klabu zote zinazoshiriki zimetoka kwenye ligi zenye changamoto na kila moja imejipanga kuendeleza makali yake hasa baada ya kuondolewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Wakati huo huo, Musonye alisema kwamba nchi wanachama zimetakiwa kujiandaa kuomba uenyeji wa mashindano ya Kombe la Chalenji ambayo yatafanyika kuanzia Novemba mwaka huu.
Musonye alisema kwamba sekretarieti itaanza kupokea maombi lakini amewakumbusha viongozi kushirikisha serikali za nchi zao ili kufanikisha mchakato wa kupata wadhamini.