come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA WAANZA KUTIMUANA, LIEWIG ATUPIWA VIRAGO, KIBADEN MRITHI

Kocha wa Simba, Patrick Liewig
 
Wakati kocha wa Simba, Patrick Liewig, akitarajiwa kuondoka nchini kurejea kwao mwishoni mwa wiki, gwiji wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni 'King' ametajwa kuwa mrithi wa mikoba ya Mfaransa huyo ambaye amemaliza msimu wa Ligi Kuu ya Bara juzi kwa kupata kichapo cha magoli 2-0 kutoka kwa watani wao Yanga.


Kibadeni ambaye alikuwa akiifundisha Kagera Sugar na hana mkataba mpya ametajwa kukabidhiwa Simba na mtihani wake wa kwanza ni kuiongoza timu kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yatakayofanyika Sudan hivi karibuni.

Abdallah Kibaden

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa Simba zinaeleza kuwa Liewig baada ya kukatiwa tiketi na kupewa mshahara wake wa mwezi Mei, atarejea kwao na barua ya kumtimua kazi ataipata kwa njia ya mtandao akiwa Ufaransa.

Chanzo hicho kiliendelea kusema kwamba bado kuna mawazo tofauti kuhusiana na kocha atakayesimamia timu lakini Kibadeni anapewa nafasi kubwa na hiyo imetokana na makocha wa kigeni kuigharimu fedha nyingi klabu kika wanapotaka kuachana nao.

Mbali na Liewig, Julio pia hatma yake bado haijajulikana kwa sababu baadhi ya viongozi wanamuhitaji huku wengine wakipinga beki huyo wa zamani kuendelea kuwapo kwenye timu.
Kibadeni alipotafutwa jana alisema "Simba ni nyumbani kwangu".

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ambaye pia ni mchezaji pekee katika historia kufunga 'hat-trick' katika mechi ya wapinzani wa jadi dhidi ya Yanga, aliongeza: "Niko huru, Siwezi kukataa wito. Simba wakiniita kwa ajili ya mazungumzo niko tayari."

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alishindwa kukataa na kuthibitisha mipango hiyo ya klabu na kueleza kuwa kwa sasa wanataka kukamilisha kwanza zoezi la usajili wa wachezaji.

Mtawala alisema ni kweli Liewig na beki wa Mali, Komalbil Keita, wanaandaliwa malipo yao na baada ya hapo kinachofuata ni kujua timu itaingia kambini lini kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame.

"Tumepokea barua kutoka CECAFA tangu Ijumaa lakini nitaijibu kesho (leo) Jumatatu, kwa sasa wachezaji wataenda likizo fupi na baadaye watarejea kuanza kujifua, suala la kocha litajulikana baadaye kidogo," alisema Mtawala.

Aliongeza kwamba licha ya timu yao kumaliza kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, bado wanaamini wana kikosi chenye wachezaji wenye vipaji na watakaosumbua msimu ujao.

Mapema mwaka huu uongozi wa Simba ulimtimua aliyekuwa kocha wake mkuu Milovan Cirkovic kwa njia ya barua pepe lakini Mserbia huyo aliyereja nchini kudai haki yake.