Kocha wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu huu wa 2012/13, Ernie Brandts
Brandts alitarajia kupanda ndege ya Shirika la Ndege ya KLM jana usiku na kwenda kwao Amsterdam ambapo ataungana na familia yake inayoishi kwenye jiji hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana alisema kwamba amewapa wachezaji wake likizo ya muda wa wiki mbili na baada ya hapo watarejea kwenye timu kujiandaa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ambayo mwaka huu yamepangwa kufanyika nchini Sudan kuanzia Juni 18 hadi Julai 2.
Kocha huyo alisema kwamba anaamini muda wa mapumziko alioutoa utawapa wachezaji wake nafasi ya kurejesha nguvu na watakapoanza tena mazoezi wawe na nguvu mpya.
Alisema mafanikio ya kutwaa ubingwa na kuifunga Simba yametokana na juhudi za wachezaji kujituma katika mchezo huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu zote mbili.
"Tunakwenda mapumziko na tukirudi tunaamini kila mmoja atakuwa na morali mpya, kuna mashindano ya Kagame ni magumu na yenye changamoto kwa sababu tutakutana na timu zinazocheza ligi mbalimbali," alisema kocha huyo.
Aliongeza kuwa tayari ameacha mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji katika msimu ujao wa ligi na akiwa kwao ataendelea kufanya mawasiliano na viongozi ili kuhakikisha zoezi la usajili linatekelezwa vyema na wajumbe wa Kamati ya Usajili.
Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema pia wachezaji wageni wa timu hiyo ambao ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite wa Rwanda, Hamis Kiiza (Uganda), Didier Kavumbagu (Burundi) na Yaw Berko wa Ghana wataondoka wakati wowote kuanzia leo baada ya taratibu zao za kiutawala kukamilika.
Yanga watashiriki michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu kama mabingwa watetezi wakati watani zao Simba wataingia wakiwa mabingwa wa msimu uliopita.