Na Anko Matua
WIKI iliyopita nilijaribu kumpa sifa yake rais wa TFF Leodegar Tenga ambaye anamaliza muda wake muda si mrefu, Tenga amefanya kitu kimoja cha kufurahisha hasa baada ya kukabidhi mipira zaidi ya 30,000 kwa ajili ya kuendeleza soka la vijana hapa nchini.
Na nimejaribu kutembea maeneo mbalimbali ili kuona kama kuna mwito kwa wadau wa soka kuendeleza soka la vijana, Simba SC, Yanga, Azam na timu nyinginezo zinazoshiriki ligi kuu zimekuwa zikitilia mkazo maendeleo ya soka la vijana na faida yake imeanza kuonekana.
Tabata Football Academy kituo cha soka kilichopo maeneo ya Tabata ni mfano bora wa kuigwa baada ya kuona jitihada zao za kuendeleza mchezo huo zikizidi kupanda ngazi moja kuelekea nyingine.
Nilibahatika kufika katika kituo hicho na kujionea mwenyewe vijana chini ya umri wa miaka 10-15 wakisakata soka pamoja na wale wenye umri wa miaka 15-17 nao waking'ara mazoezini.
Vijana hao mbali ya kuonyesha vipaji vyao pia wamepata fulsa nyingine ya kujiwekea malengo ya baadaye ya kimaisha kwani siku zinavyozidi kusonga mbele mchezo wa soka nao unazidi kubadili maisha ya vijana na kuwa moja ya sehemu ya ajira.
Vijana hao pia wanapata nafasi ya kujenga miili yao kwani mazeozi yamekuwa msaada mkubwa kwa afya ya mwanadamu na kuondokana na maradhi yote nyemelezi.
Michael Christian Meneja wa timu hiyo alisema kuwa mawazo yao ndiyo yaliyowasukuma kuanzisha timu hiyo na kuwakabidhi watu wa Tabata, Ameongeza kuwa timu hiyo sasa si mali yao binafsi na amewataka wakazi wa Tabata kuisaidia kwa hali na mali.
Aidha Michael aliongeza kuwa amekuwa akipata changamoto nyingi kutoka kwa wazazi wa watoto hao ambao wamekluwa na tabia ya kuwazuia watoto wao kutoshiriki michezo, 'Kituo changu kina jumla ya watoto zaidi ya 60, Na tulipoanza tulikuwa zaidi ya 60 lakini baadhi ya wazazi wamewazuia watoto wao wasishiriki michezo', alisema.
Lakini amefafanua kuwa si wote wenye tabia hiyo ila bado amekosa ushirikiano kutoka kwa wakazi wa Tabata, 'Ushirikiano ni mdogo tena sana timu yetu mpaka sasa imekosa wafadhili wakutusaidia, tunasumbuliwa na ukosefu wa vifaa vya michezo kama vile jezi, mipira nk', aliongeza Michael.
Timu hiyo ya vijana kwa sasa inasaidiwa na ndugu Christopher Makombe ambaye amekuwa akijitolea mara kwa mara, Makombe ameridhishwa na vipaji vya vijana hao baada ya kuwaona wakisakata soka.
Kitu kingine ambacho kimesemwa na Michael ni kuhusu ukosefu wa uwanja wa kufanyia mazoezi vijana wake, 'Timu yangu inafanya mazoezi kwenye uwanja wa shule ya msingi Tabata lakini uwanja huo unatumiwa na zaidi ya timu mbili', aliendelea kusema.
'Inatuwia vigumu kutimiza malengo yetu kwa haraka lakini tunajitahidi hivyo hivyo, Malengo yetu ya baadaye kuhakikisha vijana hawa wanakuwa na msaada mkubwa kwenye timu yetu ya taifa', alisema Michael.
Timu hiyo ilianzishwa mnamo tarehe 10 mwezi wa 10 mwaka 2012 na imekuwa na mafanikio mbalimbali kisoka, Mpaka sasa imeshashiriki miochuano zaidi ya mitatu na kuishia nafasi ya pili mara mbili na tatu mara moja.
Vijana waliopo katika kikosi hicho wanacheza kwa kujituma wakiamini ipo siku wataweza kufika mbali, Michael aliwataja waasisi wa timu hiyo ambayo tayari meshapata katiba yake ni pamoja na yeye mwenyewe ambaye ni meneja, Chriss Chitam kocha, Hussein Simba ambaye ni mratibu na mlezi wao ndugu Makombe.
Mikakati yao mikubwa kuhakikisha timu yao hiyo inafikia mafanikio iliyofikiwa na timu nyingine zinazofanya vizuri kwa sasa, Amesema kuwa wanaiendesha kisasa na tayari wamefungua email yao yamawasiliano na watu mbalimbali.
Naye katibu mkuu wa timu hiyo Fai Muya amesema kuwa timu yake hiyo inataka kuwa moja kati ya taasisi zinazozalisha vipaji hapa nchini, 'Lengo letu kujikita kitaifa zaidi na tumeanza na anuani ya mawasiliano', alisema Muya.
Aliongeza kuwa timu yake haina wafadhili, 'Unajua kuendeleza soka kunahitaji fedha, Kwa sasa hatuna fedha na ndio maana tunashikana mashati ili kuchangishana fedha ili tupate mahitaji muhimu', aliendelea.
'Makombe ni mdau wa soka ameridhishwa na vipajio vya hawa vijana lakini bado tunaendelea kuwataka wakazi wa Tabata ambao wataguswa na timu hii na wajitokeze kuisaidia, Timu yetu haina itikadi ya chama cha siasa, wala klabu yoyote ile nchini pamoja na nje ya nchi', alisema Fai.
Hata hivyo uongozi wa Tabata Football Academy wamesema kuwa timu yao bado ni changa lakini kama wakipata ushirikiano wa kutosha wanataka kufanya ziara angalau nje ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kucheza mechi za kirafiki ili kujitangaza zaidi.
Pia wanataka watembelee Zanzibar wakajumuike na timu za huko ili kudumuisha muungano, Uongozi huo umewataka wakazi wa Tabata kutoiacha timu hiyo kwani ni mali yao.
Huenda timu hiyo ikabahatika kupewa zawadi ya mipira itakayotolewa na shirikisho la kandanda nchini TFF, Mipira hiyo imetolewa na rais wa TFF Leodegar Tenga kwa ajili ya kuendeleza soka la vijana nchini