KAMA kuna timu iliyotaabika kwenye nafasi ya ulinzi ni Simba.
Timu hiyo kwa karibu mwaka mmoja sasa imekuwa ikipepesuka hasa baada ya
kuondoka mchezaji wao Kelvin Yondani aliyejiunga na Yanga.
Wachezaji ambao wamekuwa wakisajili kwenye nafasi
hiyo wameshindwa kuhimili vishindo na kufanya ukuta wa Simba kuyumba
kila mara na kufanya timu hiyo ishindwe kushindana kisawa sawa.
Lawama kubwa zimekuwa zikielekezwa kwenye kamati
ya usajili kwa maelezo kuwa imekuwa ikifanya mambo kwa mazoea kuliko
utaalamu katika kutafuta wachezaji, hususani wa kuziba nafasi hiyo ya
ulinzi.
Tayari imewajaribu mabeki saba kucheza nafasi hiyo
lakini wamechemka na kujikuta wakitupiwa virago ingawa wengine waliamua
hata kuvunja mikataba yao kuhamia klabu nyingine.
Lino Musombo (Congo)
SIMBA ilidai imepata mtu sahihi kumaliza tatizo la
kuondoka kwa beki wake wa kati, Kelvin Yondani ingawa baada ya muda
mfupi alitupiwa virago.
Lino alikuwa ameenda hewani vizuri na mwili mkubwa
ambao unamwezesha kukabiliana na kashikashi zozote uwanjani. Ingawa
Simba hawakuwa na subira ya kumvumilia na kuamua kumtupia virago.
Simba walifanya uamuzi wa haraka kwa lugha rahisi
walikurupuka katika kufanya uamuzi wa kumtimua beki huyo kwani kadri
muda ulivyosonga alizidi kuimarika kiuchezaji.
(Kenya)
MKENYA ambaye ameenda vizuri hewani na umbo kubwa.
Ni wazi umbo lake linawatisha mastraika kumpita ingawa kuna jambo pekee
ambalo limemfanya beki huyo wa kati aliyewika na timu ya Taifa ya Kenya
‘Harambee Stars’ aonekane kuwa hawezi kuendelea kuitumikia Simba na
kutupiwa virago.
Kwa mujibu wa benchi la ufundi la Simba lilidai
kuwa sababu kubwa ya kumtema kitasa huyo ni kushindwa kuendana na kasi
ya baadhi ya washambuliaji wa timu za Ligi Kuu Bara.
Ochieng aliuachia mwili wake na kumfanya awe
mzito. Aliyekuwa Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alimtaka beki
huyo kufanya mazoezi magumu kwa ajili ya kukata mwili huo.