YANGA imeamua kusuka kikosi chake cha Ligi ya Mabingwa Afrika
kwa kuanzia na nchi mbili zilizoko kwenye tano bora ya Afrika kwenye
viwango vya Fifa na itaingia kambini rasmi Julai 3 ikipiga kambi ya wiki
mbili jijini Mwanza ambako kuna uwanja mzuri wa CCM Kirumba.
Mabingwa hao wa Tanzania wamekabidhiwa majina matatu na wakala waliyempa kazi ya kuwatafutia wachezaji wa kigeni.
Mastraika wawili ni kutoka Nigeria ambayo ni ya
nne Afrika na 31 duniani na mwingine ni wa Ghana iliyoko nafasi ya pili
Afrika na ya 21 duniani kulingana na viwango vipya vya Fifa vilivyotoka
mwezi huu.
Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga, Abdallah Bin Kleb
licha ya kutotaja majina ya wachezaji hao kwa madai kuwa bado
hawajafikia muafaka, alisema wamepewa masharti na matakwa ya wachezaji
hao na kwamba wanajadiliana kabla ya kupata muafaka wa jina mmoja.
Bin Kleb alisema lengo lao kubwa ni kupata straika
mwenye nguvu, machachari, umri mdogo, akili ya kufunga na mpambanaji
kama ilivyokuwa kwa Mzambia Davies Mwape ambaye aliachwa msimu uliopita
kutokana na umri.
Kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa ndani ya
Yanga alisema wamepania kusajili mchezaji kwa kuangalia ubora wa nchi
yake na wako tayari kumlipa ilimradi ajue kutumbukiza langoni.
“Hatutamtangaza mchezaji, tunataka kufanya kama
ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa ambao walitambulishwa
wakiwa tayari wamesaini mkataba na klabu yetu, tupo makini sana katika
suala hili,” alisema Bin Kleb.
“Unajua madhara yake, unaweza kuharibu mikakati
yako ya kumpata mchezaji huyo, sisi tuna wakala siku hizi ambaye
anafanya kazi hiyo kama klabu za Ulaya, wakala wetu akikamilisha
mazungumzo na kukubali ofa yetu, tutasaini mkataba na kuweka mambo
hadharani kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine,” alisema.
Alisema kuwa wachezaji hao ni wazuri na
wanalingana kwa viwango vyao, ila jambo ambalo limewafuraisha ni jinsi
walivyokuwa wapambanaji uwanjani na hasa katika kufunga mabao.
“Tunataka mabeki wakitoka uwanjani wawe
wanasimulia wenyewe kuwa wamekumbana na straika mwenye kila kitu au
akitoka mapumziko asiwe na hamu ya kurejea tena uwanjani kipindi cha
pili, huu ndiyo mkakati wetu kwa sasa na tunataka timu ya Ligi ya
Mabingwa Afrika na wala si vinginevyo,” alisema.
Alisema Yanga itaondoka Julai 3 kwenda Mwanza kwa ajili ya kambi na mechi za mazoezi na watakaa huko kwa muda wa wiki mbili.
Kama Yanga, itampata straika huyo ina maana kuwa
kati ya Yaw Berko au Kabange Twite itabidi aondolewe katika orodha ya
wachezaji wa kigeni ili kubakiwa na watano tu.