Mwimbaji na mtunzi nyota wa muziki wa dansi nchini, Rogert Hegga 'Katapila' (Pichani) ameanzisha bendi yake ii
Hegga ambaye hivi karibuni aliachana na bendi ya Extra Bongo inayomilikiwa na swahiba wake Ali Choki, amewajumuisha kundini mwake mwimbaji Hamis Amigolas, mpiga kinanda Victor Mkambi na rapa Msafiri Diouf, wote wakiwa ni nyota waliokuwa wakiing'arisha Twanga Pepeta.
Akizungumza jana, Hegga alisema wamewajumuisha wanamuziki nyota nchini kwa nia ya kuona kuwa bendi yao inaanza kazi ikiwa juu kwa ubora na hivyo kuwa na nafasi ya kutoa changamoto kwa bendi nyingine kongwe nchini.
"Wapo wanamuziki kutoka bendi nyingine ambao tutawatangaza siku si nyingi baada ya kukamilisha mambo kadhaa muhimu... lakini hao niliowataja tayari tumemalizana nao kwa kila kitu," alisema Hegga.
Hegga alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu watakuwa tayari wameshaweka mambo yote hadharani, ikiwa ni pamoja kutangaza uongozi kamili wa bendi hiyo ambayo itapiga zaidi muziki wa hotelini.
Hegga ametangaza kuanzisha bendi ikiwa ni takriban mwezi mmoja sasa tangu aachane na Extra Bongo aliyodumu nayo kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kujiunga akitokea Twanga Pepeta.
Uongozi wa kampuni ya Aset inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta umekiri kuwapo kwa taarifa za wanamuziki wake hao kujiunga na Hegga, huku wakiwa wameahidi kuaga rasmi mara baada ya mipango yao kukamilika.
"Waliahidi kuaga ingawa hadi sasa bado hawajafanya hivyo, lakini nina uhakika wataaga tu," alisema meneja wa Aset, Hassan Rehan.