Aliyekuwa rais wa Misri, Hosni
Mubarak, amefikishwa mahakamani, siku tatu baada ya kuachiliwa huru
kutoka gerezani na kuwekwa katika kifungo cha nyumbani.
Mubarak amefunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji wakati wa mageuzi yaliyomuondoa madarakani mwaka wa 2011.
Rais huyo wa zamani alifika kizimbani akiwa na wanawe wawili wa kiume, waziri wa zamani wa usalama wa ndani na maafisa sita waandamizi wa ulinzi wakati wa utawala wake.
Awali, kesi nyingine inayomkabili generali mkuu wa vugu vugu la Muslim Brotherhood na manaibu wake wawili ilihairishwa.
Mahakama hiyo ilisikiliza kesi hiyo kwa muda mfupi na kuchukua uamuzi huo kwa sababu Mohammed Badie, Khairat al-Shater na Rashad Bayoumi hawakuwa mahakamani kwa sababu za kiusalama.
Watatu hao waliamriwa kufika mahakamani tarehe ishirini na tisa mwezi huu wakati kesi yao itakaposikilizwa.
Viongozi wa chama cha Muslim Brotherhood wanakabiliwa na mashitaka ya kuchochea mauji ya waandamanji waliovamia makao makuu ya vugu vugu la Kiisalamu mjini Cairo tarehe thelathini mwezi Juni mwaka huu, wakati mamilioni ya raia wa nchi hiyo walipoandamana kutaka kujiuzulu kwa mrithi wa rais Hosni Mubarak, aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Morsi.
Lakini kiongozi huyo aliondolewa madarakani siku tatu baadaye na viongozi wa jeshi la nchi hiyo.
Morsi anazuiliwa na utawala wa kijeshi huku viongozi wa mashitaka wakiendelea na uchunguzi kubainisha jinsi alivyotoroka kutoka kizuizini wakati wa mageuzi yaliyomuondoa rais Mubarak madarakani na madai ya kupanga njama na kundi la kigaidi la Kiislamu nchini Palestina la Hamas.