come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA KUKATA RUFAA KUTAKA SIMBA NAYO IFUNGIWE



Yanga ya jijini Dar es Salaam inajiandaa kukata rufaa dhidi ya maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya kumfungia winga wao Mrisho Ngasa na inataka Simba pia ifungiwe kusajili kwa kosa la kuingia mkataba na mchezaji huyo wakati ikijua alikuwa na mkataba na Azam.


Ngasa amefungiwa kucheza mechi sita na ametakiwa kurejesha fedha za usajili alizopewa na klabu ya Simba Sh. milioni 30 na fidia ya asilimia 50 ya kiasi hicho alichopewa na kusaini mkataba na Wekundu wa Msimbazi wakati akitokea Azam kwa mkopo.

Ngasa, ambaye ameruhusiwa kuichezea Yanga msimu ujao, alianza kuitumikia adhabu hiyo juzi ambapo aliishuhudia kutokea jukwaani timu yake ikitwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam 1-0.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb (Pichani), alisema kwamba baada ya kumaliza maandalizi ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii ambao walishinda, leo wanakutana kujadili adhabu ya Ngasa na hawakubaliani nayo.

Binkleb alisema kwamba ushindi wa mechi ya majuzi ulikuwa ni muhimu zaidi na sasa wanaelekeza nguvu zao katika kupinga adhabu aliyopewa mchezaji wao.

"Suala la Ngasa tuliliweka kiporo, tuliona hatuwezi kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja, tumemaliza mechi ya Ngao ya Jamii, sasa tunaelekeza nguvu katika kujadili jambo hilo ambalo tunaamini kwa upande wetu hatukukurupa katika kumsajili," alieleza Binkleb.

Kiongozi huyo alisema kuwa wanaamini adhabu ya mchezaji huyo itaondolewa na Jumamosi katika mechi dhidi ya Ashanti United atashuka uwanjani.

Simba pia iliwasilisha jina la Ngasa katika usajili wake wa msimu huu wa mwaka 2013/ 2014 na nakala ya mkataba alioingia mwaka jana wakati anajiunga na timu hiyo akitokea Azam.

Ili kusaini mkataba huo, Ngasa alipewa Sh. milioni 30 na gari jipya aina ya Toyota Verossa (iliyokuwa na thamani ya Sh. milioni 18) ili kuitumikia klabu hiyo.

Kiongozi mwingine wa Yanga (jina tunalihifadhi) alisema kwamba ili adhabu hiyo ya Ngasa waitambue ni lazima watani zao nao wafungiwe kusajili kwa muda wa miaka miwili.

Kiongozi huyo alisema pia suala la mshambuliaji huyo kurejesha fedha ni la kipolisi na kikanuni Simba ndiyo yenye makosa kwa kumshawishi mchezaji kusaini mkataba mpya hali ya kuwa alikuwa hajamaliza mkataba na Azam.

Suala hilo la Ngasa linatarajiwa kutua katika Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF).