KLABU ya Galatsaray ya Uturuki imesema Manchester United ilitoa ofa ya kumnunua kiungo wake mwenye umri wa miaka 29, Wesley Sneijder (Pichani).
United awali ilikaribia kumsajili kiungo huyo Mholanzi kutoka Inter Milan mwaka 2011 kwa dau la Pauni Milioni 35, lakini iliamua kuachana na Sneijder baada ya kutaka mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki.
Pamoja na hayo, sasa inasemekana United ilifufua mpango wa kumsajili mchezaji huyo chini ya kocha wake mpya, David Moyes, huku Galatasaray ikisema klabu hiyo ya Old Trafford ilimgeukia Sneijder baada ya kukwama kuwasajili Cesc Fabregas na Thiago Alcanatara mapema majira haya ya joto.
Mratibu wa Michezom, Bulunt Tulun ameliambia gazeti la Uturuki, Milliyet kwamba: "Sneijder amepokea ofa kutoka Manchester United wiki mbili zilizopita, lakini haikukubaliwa. Kulikuwa kuna klabu kadhaa zinamtaka, lakini kama ambavyo hatuwezi kumruhusu kuondoka Burak (Yilmaz) pia tunatakiwa kumbakiza Sneijder,"alisema.
Roma ilithibitisha United ilitoa ofa ya wazi kwa ajili ya Daniele De Rossi ya Pauni Milioni 12, ambayo ilipigwa chini pia, wakati Mktendaji Mkuu, Ed Woodward aliripotiwa kujaribu kumsajili kwa Pauni Milioni 30.5 kiungo wa Athletic Bilbao, Ander Herrera.
United pia ilikwama kumsajili mwanasoka wa kimataifa wa Ujerumani, Sami Khedira ahamie Old Trafford kutoka Real Madrid, na kiungo huyo amethibitisha mwenyewe alivyokoswakoswa na kocha David Moyes dakika za mwishoni.
United imefanikiwa tu kumsajili kiungo Mbelgiji wa Everton, Marouane Fellaini kwa Pauni Milioni 27.5, anayekwenda kuungana na kocha wake wa zamani Toffees, David Moyes Old Trafford.