NI kauli ya kushangaza kutolewa na beki wa kati kwamba anatamani kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu huu, Wakati akitoa kauli hiyo washambuliaji mahiri kama vile John Boko 'Adebayor', Kipre Tchetche, Jerry Tegete, Didier Kavumbagu wakiisikiliza kwa makini.
Kauli hiyo ilitolewa na beki wa kati wa mabingwa wa soka nchini Yanga Nadir Haruob 'Cannavaro' (Pichani) hivi karibuni ambapo amedai kwamba anataka kiatu cha dhahabu safari hii kiende kwake.
Cannavaro beki anayesifika kwa shughuri yake pevu awapo uwanjani ambapo amekuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji wakware wenye sifa za kucheka na nyavu.
Akizungumza na waandishi wa habari beki huyo alisema amepania vilivyo msimu huu kuchukua kiatu cha dhahabu ambapo sasa atakwenda kusaidia mashambulizi langoni mwa adui na kufunga.
Si mara yake ya kwanza Cannavaro kufunga isipokuwa amekuwa mmoja kati ya wafungaji mahiri wa Yanga ambao wameisaidia timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kutwaa ubingwa wa bara.
Katika mazungumzo yake na safu hii, Cannavaro amedai kwamba anaota ufungaji bora, 'Nataka kutimiza ndoto yangu ya muda mrefu tangia nitue Yanga, safari hii na mimi lazima niwemo kwenye orodha ya wafungaji bora ili nichukue kiatu cha dhahabu', alisema na kuongeza.
'Hilo kwangu si gumu kwani nimeweza kuifungia timu yangu magoli 10 katika mechi za ushindani na sitashindwa kutimiza ndoto yangu, namuomba mungu anijaalie uzima ili niwaonyeshe kazi makipa', aliendelea.
Beki huyo wa kati ambaye ni nahodha wa Yanga amethibitisha kauli yake hiyo huku akitaka kuwapiku washambuliaji sita waliopo Yanga, Yanga ina washambuliaji sita msimu huu ambao wamesajiliwa kwa lengo la kuiwezesha timu hiyo kupata mabao.
Washambuliaji hao ni Jerry Tegete, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu, Hussein Javu na Shaaban Kondo. Aidha kikosi cha Yanga kina viungo wengi wanaotumika kama washambuliaji.
Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Hamisi Thabiti, Haruna Niyonzima, Frank Domayo na Salum Telela wamekuwa wakitumika kama sehemu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayohaha kusaka ubingwa wa 25 msimu huu.
Cannavaro anauongoza ukuta wa Berlin Yanga unaosaidiana na Kelvin Yondani, Juma Abdul, Mbuyu Twite na David Luhende, hivyo safu ya ulinzi ya Yanga inaonekana kuwa imara na kuzitisha safu za ushambuliaji za timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu ya bara.
CANNAVARO ATAMBA KUTOOOGOPA MSHAMBULIAJI YOYOTE MSIMU HUU
Ukuta wa Yanga unazidi kupata jeuri si kwa sababu ya pesa za Yusuf Manji isipokuwa kujiamini tu, 'Safari hii simuogopi mshambuliaji yeyote yule, sitakubali ukuta wangu upitike kirahisi hivyo washambuliaji wakae chonjo', alisema Cannavaro.
Alidai kuwa yeye aogopi maneno yanayotolewa na mtu kwamba kuna mshambuliaji hatari anaweza kumpita kirahisi, hilo limekuja kufuatia tambo zinazotolewa na mahasimu wao Simba kwamba msimu huu wamesajili mshambuliaji hatari kutoka Burundi.
Amisi Tambwe mfungaji bora wa michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati iliyofanyika Darfur Sudan ambapo Yanga haikwenda kushiriki, 'Awaulize wenzake kwanza, sisi hatukwenda kushiriki Darfur na ndio maana wao wakachukua lakini kama tungekwenda wangeisikia kupitia rediuo', alisema na kuongeza.
'Sidhani kama nitamruhusu kufurukuta hata kidogo katika mchezo wetu wa Oktoba 20, tena natamani hata iwe leo ili nimuonyeshe kazi', aliendelea.
JOHN BOKO AKIRI CANNAVARO NI KIBOKO YA WASHAMBULIAJI
Mshambuliaji hatari wa Azam FC pamoja na timu ya taifa John Boko 'Adebayor' amekiri katika mazungumzo yake na Kabumbu kwamba Cannavaro wa Yanga ni kiboko ya washambuliaji.
'Mimi nimecheza Azam misimu yote lakini tukikutana na Yanga napata shida sana hasa ninakutana na Cannavaro, jamaa anajua kukaba amekuwa akinikaba muda wote na kushindwa kuonekana uwanjani huku jahazi la timu yangu ya Azam likizama', alisema Boko.
Boko amekiri kushindwa kwake kuifunga Yanga kunatokana na kudhibitiwa vilivyo na Cannavaro, Boko aliyasema hayo akiwa katika kambi ya timu ya taifa wakati wakijiandaa kuivaa Ivory Coast.
Cannavaro alisajiliwa na Yanga mwaka 2005 akitokea Duma ya Zanzibar, pia ni beki wa kutegemewa wa timu ya taifa ya Zanzibar pamoja na ile ya muungano Taifa Stars na amekuwa katika kikosi cha kwanza muda wote.
WADAU WAMSHANGAA POULSEN KUMWEKA BENCHI STARS
Baadhi ya mashabiki wa soka nchini wameshangazwa na kitendo cha kocha wa timu ya taifa Mdenishi Kim Poulsen kumweka benchi Cannavaro wakati ndiye beki bora aliyeiwezesha Yanga kutwaa mataji mbalimbali hapa nchini.
Cannavaro ameiwezesha Yanga kutwaa michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati mara mbili mfululizo, huku pia akiisaidia timu yake kutwaa tena ubingwa wa bara msimu uliopita, Cannavario anasifika kwa kutengeneza ukuta bora wa timu ya taifa iliyofuzu fainali za kombe la Chan zilizofanyika nchini Ivory Coast mwaka 2008.
Mbali na sifa hizo Cannavaro ameiwezesha timu yake ya taifa ya Zanzibar kukamata nafasi ya tatu katika michuano ya kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Kenya mwaka jana, Huyo ndiye Nadir Haruob 'Cannavaro je atang'ara msimu huu na kutimiza ndoto yake! ni jambo la kusubiri kisha tuone.