Uongozi wa timu ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu ya England umesema utaanza kujenga kituo cha kulea na kukuza vijana wenye vipaji vya michezo (academy) kitakachokuwa na uwanja wa kisasa jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao na serikali ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mkurugenzi wa biashara wa klabu hiyo, Gary Hutchinson alisema klabu yake kwa kushirikiana na kampuni ya uzalishaji umeme ya Symbion, wataanza ujenzi wa uwanja na kituo cha soka katika eneo la Kidongo Chekundu lililopo katika manispaa ya Ilala jijini humo.
Alisema ujenzi huo ni sehemu ya miradi waliyopanga kuitekeleza katika ushirikiano wa kibiashara wa miaka mitatu kati ya klabu hiyo na serikali ya Tanzania.
"Tumefarijika kuona ndugu zetu wa Symbion wamejitokeza kusaidia ushirikiano wetu na serikali ya Tanzania.
Tutajenga academy na uwanja wa kisasa ili kusaidia maendeleo ya michezo hasa mpira wa miguu nchini," alisema Hutchinson, ambaye alikuwa amefuatana na Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Sunderland, Clare Wilson na baadhi ya maafisa wa serikali ya Tanzania.
"Tuko kwenye hatua za mwisho za makubaliano yetu na serikali ya Tanzania. Tunatumai kufikia mwishoni mwa wiki hii tutakuwa tumeshaelewana kila kitu na wiki ijayo tutaeleza gharama za ujenzi huo," aliongeza.
Hutchinson aliongeza vilevile kuwa klabu yake pia itasaidia katika kuitangaza na kuitafutia ufadhili na wawekezaji sekta ya utalii nchini.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii (TTB), Aloyce Nziku, ambaye alikuwa amefuatana na mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini, Leonard Thadeo, alisema ushirikiano huo wa miaka mitatu utakuwa na manufaa makubwa katika kuinua sekta za utalii na michezo nchini.
Hatua hiyo ni matunda ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete aliyoifanya Juni mwaka huu kwenye makao makuu ya Sunderland nchini Uingereza ambako aliahidiwa na uongozi wa klabu hiyo kujengwa 'academy' ya kisasa kwa ajili ya kulea na kukuza vijana wenye vipaji vya michezo.