Marekani inaonesha kuwa iko
tayari kuacha kutaja hatua ya kijeshi katika azimio lolote la Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria.
Maafisa wa ikulu ya Marekani walisema kumepatikana maendeleo katika juhudi za kupata azimio linalokubalika, ambalo linaweza kujadiliwa baada ya ujumbe wa wakaguzi wa silaha za kemikali wa Umoja wa Mataifa kutoa ripoti yao Jumatatu.
Mazungumzo baina ya Marekani na Urusi kuhusu namna ya kudhibiti shehena ya silaha za kemikali za Syria yanaendelea kwa siku ya tatu.
Huku nyuma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-Moon, anasema anataraji kutafanywa duru ya pili ya mazungumzo ya amani kuhusu Syria, mwezi ujao.
Akizungumza kwenye televisheni ya Ufaransa, Bwana Ban alisema amezungumza na mjumbe wa Jumuia ya Nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi kuhusu swala hilo hapo Ijumaa na wote wawili wanaona hilo ni jambo muhimu.