come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SUNDERLAND YAIUMBUA SIMBA, YADAI HAWAITAMBUI

Uongozi wa timu ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu ya England umesema hauna ubia wa ushirikiano na Simba licha ya uongozi wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam kukaririwa mara kadhaa wakitamba kuwa na makubaliano ya ushirikiano na klabu hiyo ya Ulaya.


Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi wa Biashara wa Sunderland, Gary Hutchinson alisema klabu yake haijawahi kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na klabu yoyote ya Tanzania.

Hutchinson alisema uongozi wa Sunderland uko katika mazungumzo ya ushirikiano wa kibiashara, michezo na utalii na serikali ya Tanzania na kwamba hauna mpango wa kuwa na ubia na klabu yoyote ya michezo nchini.

Alisema kuwa kwa sasa barani Afrika Sunderland ina ubia na klabu mbili tu za Ghana na Afrika Kusini ambazo huzisaidia kwa kuzitangaza na kuzitafutia wafadhili na mawakala wa wachezaji.

"Ushirikiano ambao unaelekea kukamilika kwa sasa ni wa klabu yetu na serikali ya Tanzania baada ya kuombwa na Rais wa nchi hii (Jakaya Kikwete) alipotembelea uwanja wetu wa Stadium of Light Juni mwaka huu," alisema Hutchinson.

"Kwa sasa tuna ushirikiano na timu mbili za Afrika ambazo ni Asante Kotoko inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana na Bidvest Wits ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, " aliongeza.

Mtandao wa klabu hiyo iliyotwaa mara mbili ubingwa wa FA pia unazitaja Asante Kotoko na Bidvest Wits kuwa ndizo timu pekee kutoka barani Afrika zinazofadhiliwa na Sunderland.

Mei mwaka huu viongozi kadhaa wa Simba walikaririwa wakidai kuwa wamemshawishi mmiliki wa Sunderland, Ellis Short kukubali kuisaidia klabu yao.

Viongozi hao walidai kuwa uongozi wa klabu hiyo iliyoanzishwa 1879 umekubali wachezaji kupata nafasi ya kufanya majaribio Sunderland, makocha wao kupewa mafunzo na kujengewa kituo cha soka (academy) na uwanja wa mazoezi kwa timu za Simba za vijana.

Alipotafutwa jijini Dar es Salaam jana kuzungumzia suala hilo, Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema uongozi wa juu wa Simba ndiyo uliokwenda kuzungumza na uongozi wa Sunderland lakini bado hajaelezwa chochote juu ya yaliyozungumzwa Uingereza.

Klabu ya Simba ambayo ilianzishwa 1936 ilikuwa ikijulikana kwa jina la 'Sunderland' lakini baadaye lilifutwa kufuatia tamko la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lillilotaka kufutwa kwa majina ya 'kizungu' katika klabu zote za michezo nchini.