Kiungo wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ pamoja na beki Kelvin Yondan wanatarajiwa kuanza mazoezi mepesi baada ya daktari wa timu hiyo kuthibitisha kuimarika kwa afya zao.
Chuji aliumizwa vibaya goti lake katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ya Tanga wakati Yondani aliumia paja katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Akizungumza jana, daktari wa timu hiyo, Nassor Matuzya alisema Yondani ameanza mazoezi mepesi huku Chuji akitarajiwa kuanza mazoezi kesho (leo) sambamba na mshambuliaji Salum Telela ambaye alikuwa akisumbuliwa na nyama za paja.
Matuzya alisema kurejea kwa nyota hao kwa sasa kutapunguza idadi kubwa ya majeruhi wakiwamo Didier Kavumbagu, Nizar Khalfan pamoja na beki wa kati Rajab Zahir.
“Tayari Yondani na Zahir wameanza mazoezi mepesi na wakati wowote kocha atawajumuisha na wenzake katika mazoezi ya pamoja, lakini Chuji na Telela nao wataanza mazoezi kesho(leo),”alisema Matuzya.
Yanga itakutana na Mbeya City katika mchezo ujao wa Ligi Kuu, ambapo itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya Septemba14.