come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA NA YANGA USO KWA USO TENA DESEMBA 14

Baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga kufanyika Oktoba 20, timu hizo zitaumana tena Desemba 14, mwaka huu katika mechi maalum ya Ngano ya Hisani itakayoandaliwa na wadhamini wakuu wa klabu hizo Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro.


Akizungumza katika semina maalum kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema mchezo huo utakuwa maalum kwa ajili ya kampeni yao ya 'Nani Mtani na Jembe kati ya Simba na Yanga'.

Alisema bingwa ataibuka na Sh. milioni 100, huku mashabiki wa timu hizo wakitengewa Sh. milioni 20 ambapo zitatolewa Sh. milioni mbili kila wiki kwa mashabiki wa pande zote mbili watakaoshiriki zoezi hilo.

Alisema lengo la kuanzisha zoezi hilo ni kudumisha utani wa jadi kwa timu hizo ulioanza tangu zilipoanzishwa miaka ya 1935 na 1936 ambapo mashabiki wao wamekuwa wakijitokeza kuzishangilia kila zinapokutana.

Alisema tayari wamezungumza na viongozi wa timu zote mbili na kwamba wamekubaliana kuwa timu hizo mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, zitaanza rasmi mazoezi kwa ajili ya mchezo huo.

"Pia tumepata idhini kutoka Shirikisho la Soka (TFF) kuhusu mchezo huo," alisema Kavishe.