come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: TATIZO RAGE AU NAFASI YA NNE?

Na Fikiri Salum, 0755 522216.

KAMATI ya utendaji ya klabu ya Simba ilitangaza kumsimamisha mwenyekiti wake Alhaj Ismail Aden Rage kwa kile inachokiita m,atumizi mabaya ya madaraka, Wiki hii imekuwa na matukio ya kufanana kwenye nyadhifa za uongozi.

Imeanza kwa klabu ya Simba ambayo ilifikia maamuzi ya kumsimamisha mwenyekiti wake Ismail Rage ambaye alikuwa nje ya nchi kikazi, pia mwishoni mwa wiki hii Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimemvua nyadhifa zote aliyekuwa Naibu katibu mkuu wake Zitto Zubeiry Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma mjini kupitia chama hicho.

Ni maamuzi ya kushangaza hasa katika wiki hii, Simba ilitumia masaa 24 kumaliza utawala wa Rage sawa na CHADEMA, Lakini chama hicho cha siasa kiliwavua nyadhifa baadhi ya viongozi wake, tuachane na masuala ya siasa twende kwenye mada yetu husika.

Kusimamishwa kwa mwenyekiti wa klabu ya Simba kumeweza kuzua maswali kadhaa kwa mashabiki wa soka nchini ambao mpaka sasa wanashindwa kuelewa nini hasa tatizo, Rage ni mwenyekiti wa klabu hiyo aliyechaguliwa na kihalali na wanachama.

Ni vigumu sana kumuengua kiongozi aliyepitishwa na wanachama katika zama hizi za utawala bora, jitihada madhubuti zilizofanywa na uliokuwa utawala wa rais wa TFF Leodegar Tenga umeweza kutengua mapinduzi yoyote yanayofanyika kwenye vilabu vya soka hasa Simba na Yanga.


Njia sahihi kumpata kiongozi ni ile inayotokana na uchaguzi mkuu, Klabu ya Simba inaelekea katika uchaguzi mkuu ambao utafanyika hapo mwakani, ikiwa inaelekea katika uchaguzi mkuu, kamati ya utendaji ya klabu hiyo kwa kushirikiana na mwenyekiti wake Rage ilianza mchakato wa marekebisho ya katiba.

Wanachama wote wa Simba kupitia matawi yao husika walipaswa kutoa mapendekezo yao juu ya marekebisho ya katiba hiyo, kama hakuna haja ya kufanyika marekebisho pia ilipaswa kutolewa hoja ya namna hiyo, Mwenyekiti wa Simba Aden Rage alisitisha zoezi hilo kiasi kwamba kupelekea mshituko wa kutofanyika uchaguzi mkuu kama ulivyopangwa.

Ndipo yalipoanza kutokea malumbano ya chini chini, Rage ambaye pia ni mbunge wa Tabora mjini kupitia CCM alilazimika kusaifir njue ya nchi kikazi, akiwa nje ya nchi wajumbe wa kamati ya utendaji wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Joseph Itang'are maarufu mzee Kinesi walifanya kikao chao kilichokaa siku moja kujadili mambo kadhaa.

Moja kati ya maamuzi yao ni kumsimamisha mwenyekiti wao Ismail Aden Rage ambaye hakuwepo katika kikao hicho, Pia waliwafuta kazi makocha wa timu hiyo Abdallah Kibadeni 'King' na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Maamuzi hayo yalipokelewa kwa shingo upande na wadau wa soka nchini, wengi wameonyesha mshangao wao hasa kutokea kwa jambo hilo, hivi karibuni Rage alihusika katika usajili wa wachezaji wapya wawili wa Simba Awadh Issa Juma na Badru Ali Badru.

Kisha aliondoka nchini kuelekea Sudan Kusini, hii ni mara ya pili kwa Rage kusimamishwa akiwa nje ya nchi, inaonyesha Wanasimba hawamtaki ila wanashindwa kumwambia ukweli, mara ya kwanza aliondolewa na kundi la wanachama waliokuwa wakimpinga kiongozi huyo anayeonekana mbabe kisheria.

Hivyo kamati ya utendaji imeweza kurudia kama ilivyofanywa na wanachama, je Rage atasalia! Lakini kimtazamo kuna vitu viwili ambavyo ndivyo vinapelekea kumlalamikia Rage, kama inavyoeleweka kwa vilabu hivi vikongwe hapa nchini pindi vinapofanya vibaya lawama nyingi huelekezwa kwa viongozi na makocha.

Simba ya msimu huu ilianza ligi kwa makeke mpaka kukamata kiti cha uongozi huku ikiwa imeaicha vibaya Yanga kwa tofauti ya pointi tano, Mashabiki na wapenzi wa timu hiyo hakuna hata mmoja aliyewaza kutokea vurugu kama hizi za sasa.

Kitendo cha Simba kupokwa uongozi na mahasimu wao Yanga ndicho kilichoanza kuleta mvutano, Simba hawaitaki nafasi ya nne, wamezoea ubingwa au nafasi ya pili, pia hawataki changamoto na hii inaweza kuathili soka la Tanzania.

Mashabiki wake hawataki kabiusa kuona timu yao inafungwa au kutoka sare, na timu yao inapotoka sare na timu toka mikoani mashabiki wake wanafanya vurugu kiasi kwamba husababisha uvunjifu wa mali katika viwanja vya soka.

Imetokea hivi karibuni ambapo Wekundu hao wa Msimbazi walipotoka sare na Kagera Sugar walidiriki kuvunja viti vya uwanja wa Taifa na kutia hasara inayokadiliwa kuwa ya shilingi milioni 25 za Kitanzania, Sidhani kama vurugu mpaka kumsimamisha mwenyekiti wao Rage zingetokea endapo Simba ingekuwa nafasi ya kwanza.

Hata mawazo ya uchaguzi yasingekuwepo, Wakati Simba inamfunga Yanga goli 5-0 nani aliyewaza Rage aondolewe madarakani! Lakini leo hii Simba inacheza chini ya kiwango katika mechi moja au mbili tayari Rage na Kibadeni hawafai.

Kwakuwa ndio wenye dhamana ya Simba, imani yangu kwa Wanasimba umefika wakati wa kuangalia uwezo wa timu yao na pinzani, Waswahili wana msemo wao 'Ukimsifia baba yako ana mbuio basi msifu na anayemkimbiza', Kwa sasa soka la Tanzania limeanza kupata timu nyingine zenye uwezo na kasi.

Inaonekana sasa Simba na Yanga zijikaze haswa kutokana na soka maridadi linaloonyeshwa na timu mpya, Mbeya City na Azam FC zinaonekana zimejipanga vizuri katika ushindani dhidi ya wakongwe Simba na Yanga.

Masuala ya kubebwa hayapo tena, kama Wanasimba mlizoea kushinda kiloa mnapokutana na Kagera Sugar, au Ruvu Shooting hilo kwa sasa halipo, soka ni mchezo wa burudani kwa watazamaji lakini kwa wachezaji ni kazi.

Hivyo wachezaji wa timu zote pasipo kuangalia Yanga au Simba wanajituma kwa bidii ili wawee kupata nafasi ya kuitwa kwenye timu ya taifa, Taifa Stars, rai yangu kwa Wanasimba huu si wakati wa kuzozana na mwenyekiti wenu Rage, isipokuwa ni kipindi cha kujenga timu bora na imara.

Dirisha dogo la usajili tayari limefunguliwa tangia Novemba 15 mwaka huu na kufungwa Desemba 15, hivyo ni wakati wa kuimarisha kikosi chenu, wakati nyie mkigombana wapinzani wenu wanaziba mapengo na kutengeneza kikosi cha ushindani kisha mnapokutana nao mnaanza kusingizia migogoro iliyowakumba ndio tatizo.

Kama Simba ingekuwa inaongoza ligi yasingetokea matatizo yoyote, kwakuwa iko nafasi ya nne kila mmoja anaona tatizo Simba kuwepo katika nafasi hiyo.