KIPA chaguo la kwanza enzi za makocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio' Mganda Abel Dhaira hatimaye ameamua kufunguka na kuwapa makavu Simba akidai wamechangia kumshushia heshima yake mara tu alipoanza kuitumikia timu hiyo.
Dhaira ameyasema hayo kwa njia ya simu kutoka kwao Uganda alikokwenda kwa mapumziko ya msimu ambapo amedai kuwa tangia alipojiunga na wekundu hao heshima na umaarufu wake umeanza kuporomoka na kudai Simba si timu ya kuitumikia mchezaji mwenye malengo ya kucheza soka la mafanikio.
Ameongeza kuwa anaushangaa uongozi na mashabiki wa timu hiyo kudai kiwango chake kimeshuka wakati si kweli, 'Simba walinikuta nikiwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda tena chaguo la kwanza iweje tena nisiwe na kiwango! alisema kipa huyo na kuongeza.
'Mashabiki wa Simba hawataki timu yao isifungwe wakati Man United, Barcelona, Real Madrid na nyinginezo zinafungwa tena ni timu kubwa kabisa hapa duniani, hao Brazil wenyewe na makali yao walifungwa 3-0 na Ufaransa, naishangaa sana Simba simu inayochukia matokeo wakati yapo katika soka', aliendelea kusema Dhaira.
Ametamba kuwa yeye bado kipa bora na watu wajiandae kumshuhudia mara tu atakapoanza kucheza mzunguko wa pili, lakini pia amesikia kuwa klabu yake imepanga kumuuza, anadai hajapata taarifa kamili ila anasikia na kusoma katika mitandao ya kijamii ila akipewa taarifa yuko tayari kuondoka Simba na atafanya kazi yake ipasavyo kokote kule atakakokwenda.
Kipa huyo aliyecheza mechi 10 mzunguko wa kwanza na kuifkisha Simba katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24 huku ikiwa imeachwa na Mbeya City, Azam na vinara wa ligi hiyo Yanga ambao wana pointi 28, Dhaira ameushangaa usajili wa makipa wawili mahiri Ivo Mapunda na Yaw Berko.
Amedai makipa hao wote wamepata kuichezea Yanga kwa vipindi tofauti lakini itawawia vigumu kucheza katika kiwango cjha juu katika klabu hiyo kwa sababu Simba anawajua sana kwa kuchongachonga, 'Sidhani kama Ivo na Berko watafanya kazi yao vizuri pale, lakini nawatakia mema' aliongeza kipa huyo anayetarajia kurejea Iceland.