ILIKUWA kazi nyepesi kwa vijana wa Zdravkos Lugarusic kutumia dakika tisini kujipatia mabao yao matatu dhidi ya vijana wa Ernie Brandts siku ya Jumamosi ya wiki iliyopita wakati mechi ya kukata na shoka ya Nani mtani jembe ilipofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Macho yote ya mashabiki wa soka nchini yalielekezwa katika mchezo huo isitoshe kwa sasa ligi imesimama na michuano ya Chalenji imemalizika hivyo hakuna starehe nyingine ya kutazama zaidi ya mpambano huo unaoteka hisia za wengi.
Kabla ya kufanyika mchezo huo kila timu ilifanya maandalizi yake kujiandaa na mpambano huo pamoja na ligi kuu mzunguko wa pili, timu zote zilifanya usajili wa maana ili kuimarisha vikosi vyao, Yanga iliamua kuwasajili Juma Kaseja, Hassan Dilunga na Emmanuel Okwi.
Usajili wa Okwi umeweza kuzua gumzo kutokana na mchezaji huyo kuwahi kuichezea Simba kipindi kilichopita kabla ya kuuzwa kwa Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo hata hivyo haijailipa Simba hadi sasa fedha za usajili wa nyota huyo.
Hivyo usajili wake Yanga umeweza kushangaza wengi, Okwi alipokelewa na umati mkubwa wa mashabiki wa Yanga ambao walionyesha kufurahishwa na usajili wake huku wakiwabeza mashabiki wa mahasimu wao wakubwa katika soka hapa nchini Simba.
Lakini Simba nao wamefanya usajili mkubwa tena wa maana ambao umeweza kukosha nyoyo za mashabiki wa timu hiyo ambao tayari walianza kuikatia tamaa timu yao ambayo ilijiingiza kwenye mgogoro wa kiuongozi, Simba iliwasajili makipa wawili waliowahi kuitumikia Yanga katika vipindi tofauti ambao ni Yaw Berko na Ivo Mapunda.
Pia iliwasajili Awadh Juma aliyekuwa anaichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro, Badru Ally (Suez Canal) ya Misri na beki wa kimataifa wa Gor Mahia ya Kenya Donald Musoti, usajili huo umeisaidia sana Simba katika mechi yake ya mtani jembe dhidi ya Yanga.
Mbali ya kusajili nyota hao Simba imemchukua aliyekuwa kocha wa Gor Mahia Zdravkos Lugarusic ambaye ameliimarisha vyakutosha benchi la ufundi la klabu hiyo, sasa mioyo ya mashabiki wa Simba iko saafi.
Tukielekea katika mchezo wa Nani mtani jembe ambao umezua maswali kadha wa kadha huku wengi wakihoji kulikoni Yanga iliyosheheni mastaa mbalimbali wanaotikisa katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati ikakubali kupokea kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 3-1 kutoka kwa wachezaji wa kawaida sana wa Simba.
Ukimwangalia mchezaji mmoja mmoja wa Yanga utakubaliana na wengi kuwa nini kilichangia Yanga kupoteza mchezo huo, je Yanga waliidharau mechi hiyo? unaweza ukakubaliana na usemi huo kuwa Yanga waliidharau mechi hiyo kwa sababu hakukuwepo kwa aina yoyote ya dalili za maandalizi ya kutosha ya kumfunga Simba.
Imezoeleka Yanga kuweka kambi Pemba pindi inapokaribia kucheza na Simba, lakini mechi hiyo ya kirafiki haikupokelewa vema na Wanayanga, Yanga iliamua kuendelea na mazoezi ya kawaida pale katika viwanja vya Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Huku wenzao Simba wakipanda boti kuelekea Zanzibar, Simba ilipata mbinu mbadala ya kuifunga Yanga mabao hayo matatu kwa moja, kwa sasa Wanayanga wanaulizana kuhusu kipigo hicho huku maneno ya vitisho yakianza kutolewa kutoka kwa baadhi ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Kunyoosheana vidole nako kumechukua nafasi ambapo kocha wa timu hiyo Ernie Brandts anapigiwa hesabu za kutimuliwa, kama ilivyo kwa mechi za watani hao lazima mmoja anapofungwa lawama huelekezwa kwa mchezaji au kocha, ikumbukwe timu hizo zilikutana mwezi Oktoba 20 mwaka huu katika uwanja huo huo wa Taifa ambapo zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3.
Yanga ilianza kufunga mabao 3 katika kipindi cha kwanza lakini Simba ilisawazisha yote kipindi cha pili, baada ya kumalizika mechi hiyo Yanga ilimnyoshea kidole kipa wake Ally Mustapha 'Barthez', Nadir Haroub 'Cannavaro' na kiungo Athuman Idd 'Chuji', lakini aliyekumbwa na zigo la lawama ni Barthez ambaye hadio sasa anasota benchi.
Yanga ikaamua kumweka kando kabisa Barthez ambaye alikuwa nambari moja wa kutegemewa, usajili wa Juma Kaseja umelenga zaidi kuimarisha safu ya ulinzi hasa golikipa baada ya kutokuwa na imani na Barthez, na kwa upande wa Simba vile vile hawakuwa na imani na kipa wao Abel Dhaira.
Ambapo wameamua kumuacha na kuwasajili Ivo Mapunda na Yaw Berko, iliwatimua pia makocha wake Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio' kutokana na maendeleo ya timu kufifia wakati ilikuwa ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi 5 na wanaomfuata nyuma.
NINI KILICHANGIA KUIMALIZA YANGA JUMAMOSI?
Yanga imefungwa na Simba kutokana na mfumo wa uchezaji, hakuna kumlaumu Juma Kaseja wala Kelvin Yondani, Cannavaro au Niyonzima, Yanga imefungwa mabao 3-1 kutokana na aina yake ya uchezaji kila inapokutana na Simba.
Simba wanacheza kwa kutumia pasi fupifupi huku wakiwa na kasi, mfumo wa kocha wake mpya Lugarusic au Loga wa kushambulia mwanzo mwisho ndio umechangia kuiangamiza Yanga katrika mchezo huo, Vijana wa Simba walianza kwa mashambulizi makali langoni mwa Yanga na kupelekea kupata bao lake la kwanza lililofungwa na Amissi Tambwe.
Pia waliendeleza mashambulizi ya nguvu na kujipatia penalti, kasi ile imeweza kuiletea madhara makubwa Yanga, tena nasifu jitihada za walinzi wa Yanga pamoja na kipa wao kwa kuokoa magoli mengi kwani Yanga ilikuwa inateketea kabisa siku ile, kile kipigo cha goli 5-0 ilichokipata mwaka juzi kingeweaza kujiridia tena ama zaidi ya hapo.
Mfumo wa uchezaji unaotumiwa na Yanga karibu kipoindi kirefu sasa sidhani kama kinaweza kuisaidia timu hiyo katika ushiriki wake wa michuano ya kimataifa na mzunguko wa pili unaotarajia kuanza mwakani, Yanga wanacheza soka la taratibu lenye umakini huku pasi zao zikiwa fupi fupi na ikitegemea zaidi mipira mirefu.
Lakini uchezaji wa taratibu ni rahisi kuzidiwa na uchezaji wa kasi, Simba wana kasi sana hasa anapokuwepo Ramadhani Singano 'Messi', Yanga wanacheza mipira ya taratibu anapokuwepo Haruna Niyonzima, ni ngumu sana kubadilika, tutegemee miujiza katika mfumo huu kama Brandts asipobadilika Wanayanga watazidi kulia.
Tuonane Wiki Ijayo.