KLABU ya Yanga SC imeingia Mkataba wa haki za Televisheni kwa michuano ya Afrika na kampuni ya SGM ya Kenya ambao utaanzia mechi za Raundi ya Kwanza dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam mchana wa leo, Katibu wa Yanga SC, Beno Njovu amesema kampuni ya SGM imejipa matumaini kwamba klabu hiyo itavuka Raundi ya Awali dhidi ya Komorozine ya Comoro na kwenda kukutana na mabingwa Afrika, Ahly katika Raundi ya Kwanza.
Njovu amesema kwa sababu hiyo tayari wameingia Mkataba na kampuni hiyo, ambayo utaiwezesha Yanga SC kupata dola za Kimarekani 55,000 kwa mechi moja tu ya nyumbani, zaidi ya Sh. Milioni 90 za Tanzania.
Amesema haki za matangazo ya Televisheni za mechi ya ugenini wamepewa kampuni ya MGB ya Cairo, ambayo itarusha matangazo hayo kwa nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati pekeee.
Njovu amesema kwa kampuni za Tanzania ambazo zitataka kuonyesha mechi hiyo, zitatakiwa kuwasiliana na kampuni ya SGM kupata haki hiyo.
Na kuhusu mchezo wa Misri, Njovu amesema kwamba kuwa kuwa wao watakuwa ugenini, watawasiliana na wenyeji wao ili uwezwe kuonyeshwa kwa Tanzania pekee.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa SGM Francis Gaitho amesema kwamba wana matumaini makubwa Yanga itaitoa timu ya Comoro na ndiyo maana wamechukua hatua hiyo.
Yanga SC itaanza Komorozine ya Comoro katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wakiitoa watacheza na Ahly katika Raundi ya Kwanza.
Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Febaruai 7, 8 na 9, wakati marudiano yatakuwa kati ya Februari 14, 15 na 16 February 2014.