Jose Mourinho ameonya nyota wake wa Chelsea kwamba hawawezi kuendelea kuteleza tena watakapokutana na wapinzani wao katika mbio za kushinda ligi ya Uingereza dhidi ya Arsenal itakayopigwa leo.
Mourinho anaendelea kukasirishwa na straika wa Chelsea ambao wamekuwa hawafungi na tabia ya madifenda wake kulala wakati mwingine.
Mdosi huyo wa Blues kufikia sasa hajaweza kupata dawa ya shida zinazotishia kuvuruga juhudi za Chelsea za kupigania taji la Ligi ya Premia.
Fernando Torres, Samuel Eto'o na Demba Ba wamefunga mabao matano pekee kwa pamoja kwenye ligi msimu huu, na Mourinho pia amekuwa akitema na kubadilisha madifenda wake bila mafanikio.
Chelsea walishuka hadi nambari nne kwenye jedwali Jumamosi, alama tatu nyuma ya viongozi wapya Liverpool na moja nyuma ya Arsenal walio nambari tatu.
Na huku ziara hiyo ya Chelsea uwanja wa Emirates ikiwa na umuhimu sana katika mbio za kuongoza ligi kabla ya Krismasi, Mourinho amesema wazi kwamba hatavumilia tena utepetevu wa wachezaji.
"Kama hatuwezi kuimarika katika kufunga mabao, basi lazima tuimarike upande ule mwingine (wa kujilinda),” Mourinho alisema.
“Lazima tujiimarishe tunapopoteza mpira. Hilo ni wazi.
“Hatuwezi kuruhusu wachezaji wajifiche nyuma ya kisingizio kwamba hatufungi mabao ya kutosha na wasubiri hilo lifanyike.
“Hatuwezi kuchezea hilo. Watu lazima wabadilishe akili zao na wafanye kazi zaidi.
“Kuwa timu inayocheza soka vizuri ni hatua nzuri. Kuwa timu ambayo inacheza soka vizuri na kushinda mechi nyingi ni hatua ngumu kiasi.
“Baadhi ya wachezaji wamezoea kucheza wakiwa na mpira miguuni na huwa wazuri sana katika kushambulia.
“Timu inapopoteza mpira, lazima pia wawe wazuri katika kusaidia timu.”