Meneja wa Manchester United David Moyes ametetea winga wake mchanga Adnan Januzaj dhidi ya madai kwamba huenda akajilimbikia sifa ya kujiangusha ovyo.
Mchezaji huyo wa umri wa miaka 18 alionyeshwa kadi kwa kujifanya kwamba ameangushwa kipindi cha kwanza cha ushindi wa United wa 3-1 dhidi ya West Ham United Jumamosi baada ya kujiangusha alipokaribiwa na James Collins, lakini pia alifunga bao zuri na angejipatia penalti.
Hata hivyo, ingawa Moyes alikiri kwamba kadi ya njano aliyoonyesha Januzaj ilifaa, alieleza kukasirishwa kwake na hali kwamba refa Michael Jones alimwonyesha tu kadi ya njano difenda West Ham George McCartney baada yake kumchezea visivyo Javier Hernandez kwa kumgonga tindi ya mguu dakika za mwisho za mechi.
"Yeye (Jones) aliona kuigiza katika tukio jingine, lakini hakuona hilo,” akasema Moyes.
"Ninafikiri Adnan alikuwa akitarajia akabiliwe na (James) Collins, lakini ukiangalia mechi mbili zilizopita, kiasi cha vipigo alivyopata, aligongwa mara nyingi kushinda mchezaji yeyote mwingine.
“Kwa hivyo tutazungumza naye, lakini nanyi (wanahabari) huenda mnashambulia mtu asiyefaa leo.
“Nilisema wiki iliyopita kwamba kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimgonga, kwa sababu ni mtelezi sana, hupoteza watu wengi anavyocheza, na hili linaweza kufanya madifenda wamgonge.
“Lakini ni marefa wanaofaa kufanya uamuzi ufaaona natumai kwamba hatagongwa vibaya kabla ya marefa kufanya uamuzi sahihi.
Danny Welbeck na Ashley Young aliyetoka benchi pia walifungia United kabla ya West Ham kufunga moja la kufutia machozi kupitia Carlton Cole ambaye pia alitoka benchi.
Mechi hiyo ilishuhudia bao la kwanza la Welbeck Old Trafford katika kipindi cha miezi 14 na likaonyesha kuendelea kuimarika kwa United. Sasa wameshinda mechi nne katika siku 11 katika mashindano matatu, na wamefunga bao moja pekee.
Pia, ilihitimisha mkimbio wa kushindwa mechi mbili za ligi mfululizo nyumbani na Moyes alisema: "Tumeshinda mechi nyingi nzuri tangu wakati huo na ushindi wa leo (Jumamosi) ulikuwa mzuri tena, na kwa hivyo nafurahishwa sana na hilo.