come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MZUNGU AIGOMEA SIMBA, ATISHIA KUONDOKA.

Kocha mpya wa Simba, Zdravok Logarusic, raia wa Croatia ameanza kuutikisa uongozi wa Wanamsimbazi hao baada ya kuukosoa vikali Uwanja wa Kinesi na kuweka wazi kuwa haufai kwa mazoezi ya timu yake.

Logarusic, ambaye juzi alisaini mkataba mfupi wa miezi sita tu kukinoa Kikosi cha Simba, alisema baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam jana asubuhi kuwa, uwanja huo hauna sifa za kutumika kwa mazoezi ya timu ya ligi kuu.

"Uwanja huu (Kinesi) ni mbovu na haufai kwa mazoezi ya timu ya ligi kuu. Una vikwazo vingi vinavyomfanya mchezaji ashindwe kufuata maelekezo ya kocha," alisema.

"Nataka wachezaji wafanye kile nachowaelekeza lakini muda mwingi wanafanya vitu tofauti kwa hofu ya kuumia kutokana na ubovu wa uwanja. Nitaongea na uongozi kuhusu suala hili," alifafanua zaidi Logarusic.


Kadhalika Logarusic alisema ana uhakika wa kupewa mkataba wa muda mrefu kwa kuwa juhudi zake ndizo zitakazowashawishi viongozi wa Simba kufanya hivyo.
Alisema mkataba mfupi na timu hiyo usiwatie hofu mashabiki wa Simba, kwa kuwa uwezo wake ni mkubwa na atakibadili kikosi hicho jambo litakalowavutia viongozi na kumpa mpya.

"Mkataba ni mfupi sana, lakini usiwape wasi wasi kwa sababu uwezo wangu utawashawishi waniongeze muda wa kuifundisha timu hii," alisema.
Akizungumzia kwa upande wa migogoro ya timu hiyo, alisema migoro ya viongozi isiwahusishe wachezaji, kwakuwa itawaathiri katika mechi zao za mzunguko wa pili zilizosalia.

Alisema migogoro ibaki kwa viongozi wenyewe, kwani wachezaji kazi yao ni kucheza tu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mchana kuhusu suala hilo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi', aliahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya kocha huyo ambaye wameamua kumpa mkataba huo mfupi ili kuangalia uwezo wake kabla ya kumpa muda mrefu zaidi.

"Sisi kama viongozi bado hajatuambia kuhusu suala la uwanja wa mazoezi. Akishatupa taarifa rasmi, tutajua cha kufanya ili timu yetu ifanye vizuri," alisema Mzee Kinesi.

Uwanja wa Kinesi juzi na jana ulifurika mashabiki wa Simba waliotaka kuona mbinu mpya za kocha huyo wa zamani wa Timu ya Gor Mahia ya Kenya ambaye atakuwa na jukumu jipya la kuhakikisha timu hiyo inamaliza katika nafasi za juu ili kuongezewa mkataba mpya.

Ikumbukwe kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilifanya marekebisho ya Katiba yake Desemba mwaka jana na kupitisha Kipengele cha Usajili wa Klabu (Club Licensing) ambacho pamoja na mambo mengine, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeagiza timu zote za ligi kuu lazima ziwe na viwanja rasmi vya mazoezi.

Logarusic ametua Simba ikiwa ni wiki mbili tu baada ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo iliyokutana bila uwapo wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, kupitisha maamuzi ya kumsimamisha Kocha Abdallah 'King' Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu 'Julio' na kumtangaza Mcroatia huyo kuwa kocha mkuu na kwamba atasaidiwa na nahodha wa zamani wa timu hiyo ambaye kwa sasa anainoa Simba B, Selemani Matola.

Kikosi cha Simba kilianza rasmi mazoezi juzi jioni kwenye Uwanja wa Kinesi kujiandaa kwa mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga utakaopigwa Uwanja wa Taifa mwezi huu.

Simba pia itashiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mapema mwakani kabla ya kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Januari 25, mwakani wanayokamata nafasi ya nne kwa sasa.