Televisheni ya Hezbollah, Al-Manar, imesema Hassan Lakkis aliuawa karibu na nyumba yake iliyopo eneo la Hadath, kilomita saba kusini mashariki mwa Beirut.
Hezbollah inaituhumu Israel kuhusika na kifo cha kiongozi huyo.Israel haijasema lolote.
Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, kusema Saudi Arabia ilihusika katika mashambulio ya mwezi uliopita yaliyofanyika katika ubalozi wa Iran, mjini Beirut.
Iran ni nchi inayokiunga mkono kwa kiasi kikubwa kikundi cha Hezbollah, ambacho kimetuma wapiganaji wake kwenda Syria kuisaidia serikali ya Rais Bashar al-Assad katika vita dhidi ya wapinzani wa serikali yake.
Mgogoro nchini Syria umeongeza uhasama wa kidini katika maeneo ya jirani.
Taarifa iliyotolewa na Hezbollah Jumatano imesema Lakkis aliuawa akirejea nyumbani kutoka kazini karibu za sita za usiku, japokuwa haijasema namna alivyouawa.
Kikundi hicho kinasema katika siku za nyuma, Israel ilijaribu mara kadha kumuua Bwana Lakkis, lakini lishindwa.