Familia ya kandanda kote duniani inaendelea kuomboleza gwiji wa Ureno, Eusebio, atakayezikwa Jumatatu.
Mbabe huyo aliaga dunia Jumapili akiwa na miaka 71 baada ya kuugua kwa muda mrefu akisumbuliwa na matatizo ya moyo.
Eusebio alizaliwa nchini Msumbiji kama Eusebio da Silva Ferreira na anatajwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani.
Aliitumikia klabu ya mjini Lisbon, Benfica FC kwa miaka 22 ambapo uwezo wake wa mbio na kasi, kuutumia vyema mguu wake wa kulia na mbinu za kimpira kulimpa umaarufu sana nchini Ureno na kubatizwa jina la The Black Pearl or the Black Panther.
Wakati wa uchezaji wake alifunga mabao 733 katika mechi 745, pia alifunga mabao tisa kwenye michuano ya kombe la dunia ya mwaka 1966 na kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo na kuisaidia Ureno kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo.
Maelfu ya watu wanatazamiwa kutoa heshima za mwisho katika mazishi yake Jumatatu huku risala za pongezi zikiendelea kufurika kutoka voingozi na nyota mbali mbali wa mchezo alioutumikia kwa dhati.
"Kandanda imepoteza shujaa," rais wa FifaIFA, Sepp Blatter, aliandika kwa mtandao wa Twitter. "Mahala pa Eusebio kati ya magwiji hapatasahaulika."