Kocha mpya wa Yanga, Mholanzi Johannes Franciscus 'Hans' van der Pluijm, jana asubuhi alianza rasmi kazi ya kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo ambao walisema kwamba kocha huyo amekuja na mbinu mpya.
Pluijm ambaye amechukua mikoba ya Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts, jana asubuhi aliwataka wachezaji wa timu hiyo waanze mazoezi yao kwa kukimbia na baadaye kila mmoja kuchezea mpira.
Akizungumza kwa njia ya simu jana mchana, mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngasa, alisema kwamba kocha huyo mpya alikuwa akiwakumbusha kila wachezaji kujua majukumu na mipaka yake anapokuwa uwanjani.
Ngasa alisema kwamba mwalimu huyo alisisitiza sana katika nidhamu ya mchezo jambo ambalo alisema ndiyo msingi wa mafanikio.
Aliongeza kwamba wachezaji walionekana kufurahia mazoezi ya Pluijm na hapakuwa na aliyelalamikia.
"Leo (jana) asubuhi ametufundisha mengi na amesititiza kucheza kwa nidhamu uwanjani, ni mazoezi ya kawaida lakini kwa siku ya kwanza tumeanza kupokea mbinu zake, lakini si mchezo, yaani muziki mkubwa," alieleza Ngasa ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa (Taifa Stars).
Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' naye alisema kwamba kocha huyo mpya ameanza taratibu lakini wanatarajia kupata mbinu mpya kadri siku zinavyokwenda.
Alisema kwamba wanaamini uzoefu wa kocha huyo ambaye ameshawahi kufanya kazi Ghana utawasaidia kufanya vizuri katika ligi na mashindano yote ya kimataifa watakayoshiriki mwaka huu.
Alieleza kwamba kwa sasa kila mchezaji kwenye timu hiyo anajituma na hali hiyo imeongeza ushindani wa kuwania namba katika kikosi cha kwanza.
Tayari kikosi cha Yanga kimeshacheza mechi mbili na kirafiki na zote wameshinda. Katika mechi ya kwanza walishinda 3-0 dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Ankara Sekerspor kabla ya juzi kushinda 2-0 dhidi ya timu ya daraja la pili ya Fafanga Inc.
Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa ligi ya Tanzania Bara na mara baada ya kurejea nchini wataanza mechi ya mzunguko wa pili kwa kucheza dhidi ya Ashanti United Januari 25 kwenye uwanja wa Taifa jijini.