come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA KUSAKA HESHIMA UTURUKI LEO, KUIVAA ANKARA SPOR.

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga leo wanacheza mechi yao ya kwanza dhidi ya timu daraja la kwanza ya Ankara Seker Spor, huku uongozi wa timu hiyo ukiweka bayana jina la kocha mkuu leo.

Mechi hiyo itachezwa saa 9.00 za Tanzania.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mashindano ya Kimataifa wa Yanga, Seif ‘Magari’ Ahmed timu hiyo ilifanya mazoezi jana asubuhi kutokana na jua kuwahi kuzama na hali ya hewa kubadilika.

Ahmed alisema kuwa wachezaji wanaendelea vizuri na mpaka sasa wamepania kufanya vyema katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.


Alisema kuwa baada ya mechi hiyo, timu hiyo itaendelea na mazoezi kabla ya kucheza mechi nyingine mbili na timu za madaraja ya juu.

“Timu imeanza kambi rasmi, na mazoezi mazuri na maandalizi yametupa moyo japo kwa siku ya kwanza, kesho (leo) watacheza mechi ya kirafiki ya kwanza na timu ya daraja la kwanza, ni mechi nzuri kwani timu hiyo inashika nafasi za juu katika ligi hiyo,” alisema Seif.

Alisema kuwa kwa sasa timu yao inakaa mji mwingine tofauti na Antalya ambao upo kilometa 70 kutoka mji wao wa zamani.

Kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema: “Nashukuru wachezaji wote wako katika hali nzuri kimwili na kiakili. Sina shaka kwamba ziara hii itatusaidia kujiweka tayari kwa mashindano.

“Kwa kweli mazingira haya naamini timu itabadilika na kurejea nchini ikiwa katika kiwango cha ushindani,” alisema Mkwasa.

Aidha, timu ya Sivasspor iliyopo Ligi Kuu nchini Uturuki inayonolewa na mchezaji wa zamani Real Madrid na timu ya Taifa ya Brazil, Roberto Carlos pia imeweka kambi katika Hoteli ya Sueno na jana asubuhi kabla ya Yanga kuanza mazoezi waliweza kupiga picha ya pamoja na gwiji huyo.

Hii ni mara ya pili kwa Yanga kufanya ziara ya mafunzo nchini Uturuki. Ilifanya safari kama hiyo mwaka jana na iliporejea ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati huohuo; uongozi wa klabu hiyo leo utamtambulisha kocha mkuu wa klabu hiyo katika mkutano maalumu na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo.