come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

OMARI CHANGA: UMEONDOKA UNGALI UNAHITAJIKA, MISIMAMO YAKO DARASA KWA CHIPUKIZI

Na Fikiri Salum

Jina la Omari Changa si geni masikioni mwa wapenda michezo jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake, umaarufu wake umetokana na umahiri wake wa kusakata kandanda ambapo umemfanya ajikusanyie mashabiki wengi.

Amejengeka kimichezo, ana umbo zuri, urefu na nguvu ambavyo vimemfanya aogopeke awapo uwanjani, amechagua kucheza nafasi ya ushambuliaji, na bila shaka ameweza kuimudu kwani ukimpa nafasi anaitumia vyema.

Nilibahatika kumshuhudia kwenye mechi kadhaa za ligi kuu na zile za 'mchangani' jamaa ni mzuri kwakweli na ameweza kuonyesha kuwa ni mmoja kati ya washambuliaji hatari tuliobahatika kuwa nao hapa nchini.


Tanzania kwa miaka hii ya karibuni imeandamwa na mkosi wa kutokuwa na washambuliaji kama enzi zile za akina Zamoyoni Mogella, Edward Chumilla, Malota Soma, Madaraka Seleman, Said Mwamba 'Kizota', Makumbi Juma 'Homa ya jiji', Innocent Haule, Kitwana Seleman, Fumo Felician, Juma Mgunda, Mohamed Hussein 'Mmachinga' na wengineo.

Timu yetu ya taifa haikupata shida ya kuteua kikosi chake imara chenye utitiri wa washambuliaji, tangia kutoweka kizazi hicho taifa limekosa washambuliaji wenye uwezo na maarifa kama hao.

INA MAANA HAKUJATOKEA KAMA HAO?

Miaka ya hivi karibuni idadi ya washambuliaji kama akina Mogella au Kizota ilianza kupotea, timu yetu ya taifa iliyokuwa na makocha tofauti kuanzia Mbrazil Marcio Maximo,Jan Poulsen na sasa Kim Poulsen bado ina matatizo kwenye safu ya ushambuliaji.

Na katika ligi kuu ya bara idadi ya washambuliaji wazawa imeanza kutoweka, mshambuliaji wa mwisho kung'ara alikuwa John Bocco wa Azam Fc ambaye kwa sasa ni majeruhi.

Ukitembea pembe zote za nchi hakuna straika hatari wa kuifanya Tanzania ing'are kwenye soka la kimataifa, ligi yetu ya bara washambuliaji wanaong'ara wote ni wakigeni na wanalipwa fedha nyingi na vilabu vyao.

Mrudni Amissi Tambwe wa Simba,Mganda Hamisi Kiiza wa Yanga na Muaivory Coast Kipre Tchetche wa Azam FC ndio wanaong'ara kwa upachikajhi magoli katika ligi yetu huku washambuliaji wazawa wakiachwa mbali kwa ufungaji.

Si kwamba Tanzania imekosa mastraika wa kufumania nyavu, hapana, Omari Changa ndiye aliyesalia katika kundi la washambuliaji hatari kama wale wa miaka ya 90 akina Mogella na wenzake.

Isipokuwa Changa alikuwa na misimamo yake, katika uhai wake marehemu Changa hakupenda kubaguliwa hata kidogo na alitaka haki sawa kwa wote,kwa sasa Changa hatunaye ilamisimamo yake ni funzo kwa chipukizi.

Niliwahi kumsikia katika kituo kimoja cha redio ambapo alifanya mahojiano na mtangazaji wa kituo hicho.

Changa alilalamikia tabia za viongozi wa vilabu vikongwe kubagua wachezaji, utakuta kazi anayoifanya uwanjani ni kubwa lakini kwenye maslahi anapewa kidogo huku wachezaji wengine wanalipwa zaidi yake.

Hilo lilipelekea kujiondoa katika kikosi cha Yanga ambayo ilivutiwa na uwezo wake na kumsajili akitokea Vijana ya Ilala, Changa alijikuta anasusa kuichezea Yanga mara tu alipoanza kuitumikia.

Aliisaidia sana Yanga na aliweza kuonyesha makali ya hali ya juu kisais kwamba Wanajangwani walizikumbuka enzi za akina Said Mwamba 'Kizota', MNakumbi Juma 'Homa ya jiji' na nyota wengine kadhaa waliopata kung'ara katika klabu hiyo.

Marehemu Changa aliondolewa katika kikosi cha Yanga kwa madai ya utovu wa nidhamu, lakini yeye mwenyewe alidai kuwa Yanga kulikuwa na ubaguzi, kuna wachezaji hawaonyeshi uwezo wowote uwanjani lakini hulipwa fedha nyingi, alipobaini akaondoka zake.

Maisha yake aliyaendesha kwa kufanya biashara ndogondogo huku akijikita kwenye soka la mchangani, niliwahi kuzungumza naye akanithibitishia kuwa soka la mchangani ni zaidi ya ligi kuu kwa mtu kama yeye.

Anasema timu za mitaani zinamlipa 50,000 mpaka 70,000 kwa mechi moja ya ndondo na kwa wiki anaweza kucheza mechi mbili au tatu hivyo kwa mwezi ana fedha nyingi kuliko mchezaji wa ligi kuu hasa anayechezea timu zisizo na mfadhili.

Mwaka 2006 Marcio Maximo kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars alitakiwa na wadau kumjumuhisha straika huyo kwenye kikosi chake kilichokuwa kinasaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia, Waliamini Changa ndiye mwarobaini katika safu ya ushambuliaji hasa baada ya kukosekana kwa mtu mwenye uwezo wa kumzidi yeye, Changa alisifika kwa upachikaji magoli.

Mpaka anaaga dunia Changa hatosahaulika kwa magoli yake mawili aliouia Simba SC katika mchezo wa fainali ya kombe la Tusker wakati anaichezea Kagera Sugar.

Changa alifunga magoli hayo akipokea pasi kutoka kwa kiungo Mrisho Ngasa ambaye kwa sasa anaichezea Yanga, historia ya Changa inaeleza kuwa alianza kucheza soka katika klabu ya Evareth ya Temeke.

Alisajiliwa na Vijana ya Ilala ambapo Yanga ilivutiwa naye na kumsajili, marehemu Changa alipatwa na mauti usiku wa jumamosi kuamkia jumapili na maiti yake iliokotwa katika mtaro wa maji taka asubuhi ya jumapili ambapo alizikwa jumatatu wiki hii.

Hadi sasa kifo chake kina utata ambapo kwa mujibu wa familia yake wanasema mwili wa marehemu ulikutwa namajeraha na inasadikika kuwa marehemu alinyongwa, wanaeleza kuwa marehemu alikutwa kwenye mtaro lakini shingo yake ilikuwa imeregea kana kwamba wauaji walimnyonga.

Pia alichomwa na kitu chenye ncha kali tumboni kwake na kutokea upande wa pili, hapo awali ilitangazwa marehemu alipatwa namauti kutokana na ajali ya pikipiki iliyotokea katika barabara ya Jangwani na Kigogo.

Rest in peace: Omari Changa.