come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KAGAME CUP YASOGEZWA MBELE

Mashindano  ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka huu sasa yatafanyika mwezi Agosti badala ya Juni kama kalenda ya michuano hiyo ilivyo, imeelezwa.

Hata hivyo, mwenyeji wa mashindano hayo bado hajajulikana na habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) zinaeleza kuwa wadhamini bado hawajapatikana.

Tanzania na Rwanda ndiyo nchi zinazotajwa huenda mojawapo ikawa mwenyeji wa mashindano hayo kufuatia mazungumzo yanayoendelea kati ya viongozi wa juu wa CECAFA, viongozi wa Chama cha Soka cha Rwanda (FERWAFA) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema kuwa CECAFA imeamua kuyasogeza mbele mashindano hayo kwa sababu nchi nyingi sasa zimewekeza katika fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika mwezi Juni na kumalizika Julai mwaka huu.

Alisema kwamba kila nchi mwanachama wa CECAFA atajulishwa mabadiliko hayo na wanatakiwa kuandaa timu zao zitakazoshiriki michuano hiyo ya mwaka huu.

"Mashindano sasa yatakuwa Agosti, mambo mengi hayajakamilika na ni wazi Kombe la Dunia pia limechangia mabadiliko haya," alisema Musonye.

Timu ya zamani ya mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe, Vital’O ya Burundi ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambayo mwaka jana ilifanyika katika mji wa Darfur, Sudan.

Yanga waliokuwa mabingwa watetezi kabla ya Vital'O kushinda, mwaka jana hawakuenda Darfur kufuatia maelekezo yaliyotolewa na serikali kutokana na usalama wa mji huo wa Darfur.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye pia ni mlezi wa CECAFA amekuwa akidhamini mashindano hayo tangu mwaka 2002 kwa kutoa kitita cha Dola za Marekani 60,000 kwa ajili ya zawadi kwa bingwa, mshindi wa pili na mshindi wa tatu.

Rwanda ambayo iliandaa mashindano ya Kombe la Kagame mara ya mwisho ikiwa mwaka 2010 tayari imeshathibitisha kuandaa fainali za Kombe la Chalenji mwakani.