Boniface Mkwasa, kocha msaidizi wa Yanga, amesema ushindi wa mabao 3-0 ambao timu yake iliupata dhidi ya Rhino Rangers mjini Tabora juzi, umefufua matumaini ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza mara tu baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini hapa, Mkwasa alisema ushindi huo umeiwezesha timu yake kupata nguvu ya kutetea taji hilo linalowaniwa kwa udi na uvumba na vinara wa msimamo Azam FC huku Mbeya City nao wakipigana kimya kimya.
"Tumekuwa na matokeo ya sare katika mechi mbili zilizopita na zilionekana kutuvunja moyo.
Ninaamini ushindi wa leo (juzi) utaongeza morali ya kupambana kutwaa ubingwa," alisema kocha huyo aliyetua Yanga mzunguko wa pili wa ligi hiyo msimu huu akitokea Ruvu Shooting baada ya kutimuliwa kwa Felix Minziro aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo ya Jangwani.
Kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, kikosi cha Mholanzi Hans va der Pluijm cha Yanga, kiliondoka jana asubuhi mjini hapa kurejea Dar es Salaam kikijivunia kupata pointi tatu muhimu.
Mabao ya wanajangwani yalifungwa na Jeryson Tegete aliyefunga mawili na mtokeabenchini Hussein Javu aliyehitimisha kwa bao zuri la pasi murua ya mshambuliaji Emmanuel Okwi.