Boniface Mkwasa, kocha msaidizi wa Yanga, ameonyesha kutoukubali muziki wa Azam FC baada ya kudai kwamba timu hiyo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu kwa mizengwe.
Ikiwa na mechi moja mkononi, Azam FC, timu pekee ambayo msimu huu haijapoteza hata mechi moja, juzi ilitwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya na kuvunja mwiko wa wageni hao wa Ligi Kuu kufungwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Lakini, mara tu baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa huku Azam wakipata ushindi pia, Mkwasa alisema Yanga imeshindwa kutetea taji lake kutokana na mizengwe ambayo hakuiweka wazi hata hivyo.
"Tulitambua watapata ushindi Mbeya kwa sababu ya mizengwe. Timu gani inashinda mechi zote hizo ugenini kama si mizengwe," alisema Mkwasa.
Hata hivyo, Azam FC kupitia kwa Ofisa Habari wao Jaffar Idd Maganga walisema juzi kuwa: "Matukio ya soka yanaamuliwa na refa na si mtu mwingine. Tumefunga magoli ambayo marefa wameyakubali na sisi ni timu bora ndiyo maana tumefanikiwa kutwaa ubingwa."
Yanga ilipoteza 3-2 dhidi ya Azam FC mzunguko wa kwanza kabla ya kutoka sare ya bao moja mzunguko wa pili, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Septemba 29 mwaka jana na Machi 19 mwaka huu.