come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

CANNAVARO ATOBOA SIRI KUREJESHWA STARS

Nadir Haroub 'Cannavaro', beki wa kati na nahodha wa Yanga amesema mechi mbili walizocheza dhidi ya Al Ahly mwaka huu ndizo zilizomsaidia kurejeshwa tena katika kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars).

Baada ya kulala kwa magoli 3-0 dhidi ya timu ya taifa ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi, juzi benchi la ufundi la Stars linaloongozwa na Mholanzi Mart Nooij liliongeza wachezaji tisa akiwamo Cannavaro katika kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Malawi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya Jumapili.


Akizungumza kwa njia ya simu jana akiwa kwao Zanzibar, Cannavaro alisema amefurahi kuitwa tena Stars huku akiweka wazi kwamba kumetokana na jitihada zake binafsi alizozionyesha kuanzia katika mechi zao dhidi ya Al Ahly.

"Bado niko Zanzibar kwa sababu mpaka sasa sijapata barua ya kuitwa kwangu kuitumikia timu ya taifa.

Nilikuwa na wakati mgumu sana katika miezi miwili iliyopita lakini nilipata ushauri kutoka kwa watu wangu wa karibu, nikawa ninacheza kwa kujituma na kurejesha kiwango changu.

Mechi zetu dhidi ya Al Ahly zimenijengea kujiamini na kunipa heshima," alisema Cannavaro huku akiweka wazi kwamba ameongezwa mkataba mwingine Yanga.

Jana mchana Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliiambia NIPASHE kuwa taarifa za wachezaji kuitwa kwenye timu za taifa hutolewa na shirikisho hilo kwa klabu wanakotoka wachezaji husika.

"Sisi tunachokifanya ni kuitaarifu klabu anakotoka mchezaji, na kushughulikia masuala ya usafiri wa wachezaji husika," alisema Wambura.

Alipotafutwa na gazeti hili jana alasiri kuzungumzia suala hilo, Kaimu Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema: "Sisi (Yanga) kwa wiki mbili sasa hatuzungumzi chochote kuhusu soka la Tanzania, hatujaona barua ya TFF kuhusu Cannavaro."

Mbali na Cannavaro, nyota wengine walioitwa kuongeza nguvu Stars ni Edward Charles Manyama (JKT Ruvu), Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Javu (Yanga), John Bocco 'Adebayor' (Azam), Kelvin Friday (Azam), Oscar Joshua (Yanga) na Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) huku beki mwingine wa kati Kelvin Yondani wa Yanga akitemwa baada ya kushindwa kuripoti kwa wakati mwafaka.

Stars iliingia kambini jijini Mbeya jana kujiweka sawa kabla ya kuwakabili The Flames (Malawi) mwishoni mwa wiki.