Mshambuliaji wa Barcelona raia wa Brazil, Neymar atakaa nje ya uwanja kwa wiki nne, wakati naye beki Jordi Alba atakaa muda kama huo baada ya wote kupata majeruhi.
Klabu ya Barcelona imethibitisha kuwa Neymar alipata majeruhi ya mguu juzi katika mchezo wa fainali ya kombe la Mfalme dhidi ya Real Madrid.
Kinda huyo mwenye miaka 21 alishindwa kuisaidia Barca kuepukana na kipigo cha mabao 2-1, huku Mbrazil huyo akikosa nafasi ya wazi dakika za lala salama.
Neymar atakosa mechi zijazo dhidi ya Athletic Bilbao, Villarreal, Getafe na Elche.
Hata hivyo klabu ya Barca ina matumaini kuwa nyota wake huyo anaweza kurudi katika mechi ya mwisho dhidi ya Atletico Madrid.
Taarifa ya klabu ya Barcelona imesema;”Mchezaji huyu aliumia juzi katika mguu wake wa kushoto na anahitaji muda maalumu wa matibabu. Makadirio ya kurudi uwanjani ni wiki nne”.
Naye Jordi Alba alitolewa baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza katika mechi ya jana na taarifa zinaeleza kuwa beki huyo wa kushoto aliumia nyama za paja za mguu wake wa kulia.
Beki huyo wa zamani wa Valencia anaweza kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu hadi nne.