Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, atapewa nafasi finyu au asipewe kabisa nafasi tena ya kumchagua mrithi wake baada ya kutimuliwa kwa aliyempendekeza, David Moyes.
Fergie mwenye miaka 72, ambaye alitwaa mataji 38 katika miaka 26 akiwa kocha wa miamba hiyo ya Old Trafford, alipewa nafasi ya kumchagua kocha atakayerithi mikoba yake alipotangaza kustaafu msimu uliopita.
Chaguo lake, Moyes, alitimuliwa rasmi jana baada ya kikao cha asubuhi na Mkurugenzi Mtendaji wa Man United, Ed Woodward kikao kilichofanyika katika Uwanja wa Carrington, ambapo ndipo kuna makao makuu ya klabu hiyo.
Uamuzi wa kumwachia Fergie kuchagua mtu atakayekuwa sahihi kurithi mikoba yake ulikuja baada ya mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na miamba hiyo, hivyo aliaminika katika uchaguzi wake, ambapo hadi sasa bado ni balozi wa klabu hiyo akijikusanyia pauni 2 milioni kwa mwaka.
Uongozi wa Man United kwa sasa wako makini katika kuangalia makosa waliyoyafanya ya kumuacha Ferguson kuchagua mtu aliyeleta matatizo, hata hivyo, wamemchagua kiungo wa zamani, Ryan Giggs kuwa kocha wa muda, wakati Nicky Butt akiwa msaidizi wake.
Mtandao wa Sportsmail umebaini kuwa beki wa zamani aliyekuwa katika benchi la ufundi chini ya Moyes, Phil Neville, amebaki klabuni hapo.
Klabu hiyo pia inajiandaa kumrudisha mchezaji wake wa zamani, Paul Scholes, katika timu hiyo ya Old Trafford, baada ya kuondoka kwa Moyes, ambapo ilitangazwa jana asubuhi.
Scholes hakuonekana tangu alipokuwa akishirikiana na Nicky Butt katika kukinoa kikosi cha vijana chini ya miaka 19 mapema mwanzoni mwa msimu huu