Kaimu meneja wa Manchester United Ryan Giggs ana uwezo wa kufanikisha
ufanisi sawa na wa Pep Guardiola alipokuwa kocha wa Barcelona, kwa
mujibu wa kipa Anders Lindegaard.
"Huenda likaonekana kama wazo la kijinga, lakini kwa maoni yangu,
huyu ni Guardiola mpya," Lindegaard aliambia BBC Sport Jumanne.
"Yale tumeyaona wiki ya kwanza yamekuwa na ushawishi sana. Yanafanana
sana na Sir Alex Ferguson na ni wazi kwamba Ryan Giggs amejifunza
kutoka kwa mmoja wa makocha wa soka walioheshimiwa zaidi katika
historia.”
Giggs, anayeshikilia rekodi ya kuchezea United mechi nyingi zaidi,
aliwekwa kwenye usukani kwa muda wiki iliyopita baada ya David Moyes
kufutwa kazi miezi 10 pekee baada ya kuanza kutumikia mkataba wake wa
miaka sita kama mrithi wa Ferguson.
Mechi yake ya kwanza uongozini, Giggs alifanikisha ushindi wa 4-0
nyumbani dhidi ya Norwich City, na Lindegaard anasema kiungo huyo wa
kati wa miaka 40 aliwapendeza wachezaji wenzake.
"Baadhi wanaweza kuuliza maswali kuhusu kama unaweza kubadilika
kutoka mchezaji siku moja na kesho uwe meneja. Kawaida, ninaweza kuwa na
shaka pia, lakini kuhusu Giggs, mambo ni tofauti,” raia huyo wa Denmark
akaongeza.
"Hotuba yake ya majuzi zaidi, kabla ya timu kwenza uwanjani mechi ya
Norwich, ilifanya nywele zangu zisimame kwa njia ambayo niliwahi tu
kuhisi chini ya Sir Alex Ferguson: 'Msiwavunje moyo mashabiki!'"
Giggs anaripotiwa kutopigania nafasi ya kumrithi Moyes kwa njia ya
kudumu United, huku kocha wa Uholanzi Louis van Gaal na kocha wa Real
Madrid Carlo Ancelotti wakiwa miongoni mwa wanaoongoza kupigania kazi
hiyo.
Kocha wa sasa wa Bayern Munich, Guardiola alijizolea sifa kama
mchezaji wa Barcelona kabla ya kuwa kocha 2008. Aliongoza klabu hiyo
kushinda vikombe 14 kabla ya kujiuzulu miaka miwili iliyopita.