KUFUATIA usajili walioufanya Azam fc kwa wachezaji wawili wa Yanga SC, kiungo mkabaji, Frank Domayo na mshambuliaji wa kati, Didier Kavumbagu na kuzua mvutano baina ya wapenzi, wanachama na viongozi wa klabu hiyo, wachezaji wa zamani wa Yanga wamewataka wanachama kuwa wamoja na kutoruhusu migogoro kuchukua nafasi.
Domayo na Kavumbagu walisajiliwa mwanzoni mwa wiki hii ambapo Mrundi ndiye alikuwa wa kwanza kutia sahihi katika fomu za Azam akifuatiwa na Domayo siku moja baadaye.
Usajili wa Domayo uliwashitua wana Yanga wengi na kuanza kuhoji iweje uongozi umwachie aende wakati bado wanaona ana msaada mkubwa kwa klabu.
Domayo alisajiliwa akiwa katika kambi ya timu ya taifa iliyopo jijini Mbeya kujiandaa na mchezo wa leo dhidi ya Malawi katika uwanja wa sokoine, lakini si jambo jipya kwasababu hata Yanga walimsajili miaka miwili
iliyopita akiwa kambi ya Stars.
Huu ni usajili uliowagusa wapenzi wengi wa Yanga na pengine kupandisha hasira kwa viongozi wao.
Kupitia mtandao huu, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Yanga, bilionea Davis Mosha alilalamika na kuhoji kwanini wachezaji muhimu waondoke?.
Mosha alienda mbali zaidi na kusema labda kwavile viongozi wasasa wanaondoka madarakani, hivyo wanataka kuiacha timu haina wachezaji kwasababu wamesema hawagombei tena.
Mbali na Mosha, wanachama wengine wa Yanga wamekuwa wakilalamika sana kuondoka kwa nyota wao, hasa kipenzi cha roho zao, kiungo mahiri, Frank Domayo `Chumvi”.
Kutokana na hali hii kuendelea miongoni mwa wana Yanga, baadhi ya wachezaji wa zamani wa klabu hiyo wamelazimika kupaza sauti zao na kutoa maoni yao.
Katika mahojiano Maalum, mchezaji mahiri wa zamani wa Jangwani, Shaban Katwila amesema kwasasa mpira ni ajira , hivyo vijana wanapomaliza mikataba wana haki ya kutafuta sehemu nyingine yenye masilahi mazuri zaidi.
Katwila alieleza kuwa kutokana na vijana wengi kutafuta maisha, viongozi waliopo madarakani wanatakiwa kuwadhibiti wanapoona wanafaa ili wasiondoke.
“Mpira siku hizi ni ajira. Mchezaji anacheza kwa ajili ya masilahi, kama wanaelekea kumaliza mikataba, viongozi lazima wachangamkie kuwaongezea mikataba kama wapo katika mipango”.
“Wakichelewa kufanya kitu hicho, wachezaji lazima waondoke kwenda kutafuta masilahi mazuri”. Alisema Katwila.
Aidha, mkongwe huyo wa Yanga aliongeza kuwa mchezaji anapokuwa na kiwango cha juu anapanda bei na inadidi aongezewe dau,lakini inaposhindikana hawezi kuacha kutafuta sehemu yenye pesa nzuri.
“Cha msingi ni kufanya maamuzi ya mapema, wakae na wachezaji na kufanya mazungumzo juu ya mahitaji yao, vinginevyo wataleta ugomvi kwa wanachama ambao watafirikia kuwa wanapoteza wachezaji kwasababu ya uzembe wa viongozi”.
“Nilisoma sehemu nikasikia walikuwa na mazungumzo na Kavumnagu, lakini Domayo walishamalizana naye na kilichokuwa kinasubiriwa ni wakala wake ambaye ni mjomba wake, lakini bado nashangaa kaondoka”.
“Labda kuna vitu aliahidiwa na Azam fc, hii ni timu yenye pesa”
“ Na kwakuwa wachezaji wetu imewaingia akilini kuwa mpira ni ajira, asingekataa kuondoka labda kama Yanga wangepanda dau zaidi”. Alifafanua Katwila.
kavumbagu3Nyota huyo wa zamani aliongeza kuwa kwa bahati nzuri Yanga hawajapoteza sana kwasababu bado wapo katika mashindano ya kimataifa, hivyo kwa vyovyote vile wachezaji muhimu wanatakiwa kulindwa kimaslahi, kujengwa kisaikolojia ili waendelee kuwepo mpaka msimu ujao.
“Ushauri wangu; nawaomba viongozi wawe makini sana kuepuka kujenga mazingira ya kutoaminiwa na wanachama wao. Wafanye maamuzi sahihi kwa muda muafaka”.
“Wanachama wasiwe na jaziba, cha msingi wakae na viongozi wao ili suala hili liishe”. Alimaliza Katwila.
Mbali na Katwila, naye kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa stars, Waziri Mahadhi amesema hadhani kama Domayo na Kavumbagu wamekosea kwasababu mpira ni biashara.
Mahadhi alifafanua kuwa wachezaji hawa wana familia zao na maisha yao, hivyo inapotokea sehemu yenye maslahi makubwa, lazima waende na si dhambi kuondoka kwa soka la kisasa.
“Mpira umebadilika sasa hivi, sidhani kama wanapotokea watu wenye dau kubwa, mtu mwenye akili timamu hawezi kukataa”.
“Kwa viongozi , nadhani kwa kiasi fulani walifanya makosa kwasababu kama walikuwa wanawahitaji wasingewaachia kirahisi”.
“Kilichotakiwa ni kungumza nao mapema ili kuwapa mikataba mipya, lakini kusema viongozi wanaondoka ndio maana wanaachia wachezaji, mimi sina uhakika, japokuwa walifanya makosa”.
“Angalia mfano Rooney alitaka kwenda Chelsea, lakini Man United walikuwa wanamhitaji na mkataba unaelekea ukingoni, yakafanyika maamuzi ya haraka kumuongezea mkataba”.
“Tunaona wenzetu kwa wachezaji muhimu inapobaki miaka miwili wanaanza kuhangaika kuzungumza nao ili wawabakishe”.
“Lakini unashangaa eti mpaka Domayo anabakiza mwezi mmoja bado hajasainishwa mkataba mwingine, hapa viongozi nao wamefanya makosa”. Alisema Mahadhi.
Mahadhi alishauri wana Yanga kuwa watulivu na kuachana na mivutano kwasababu imeshatokea na wachezaji hawapo tena.
“Wameshateleza, cha msingi watafute wachezaji wanaofanana au zaidi ya hao ili maisha mengine yaendelee, lakini kulumbana haisaidie kitu”. Aliongeza Mahadhi.
Kuondoka kwa Domayo na Kuvumbagu kumeonekana ni pengo kubwa kwa Yanga, lakini jana mshambuliaji wa klabu hiyo, Jeryson John Tegete aliwashauri wana Yanga kuachana na hilo kwasababu waliobaki wanaweza kuipataia mafanikio kalbu.
“Tunajua walikuwa muhimu, lakini nashangaa watu wanawalaumu viongozi.
“Sio ishu kubwa sana, kawaida tu, wapo wengine watakaoonekana wakipewa nafasi zao.
“ Wasishindwe kulala kisa Domayo na Kavumbagu”. Alisema Tegete.
Dirisha la usajili bado halijafunguliwa, lakini Azam fc wameshalipua bomu kwa kugusa mitaa ya Twiga na Jangwani.