come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: YANGA- TANDALE WANAJIAMINI NINI!

Na Fikiri Salum

NIMEAMUA kuibuka na kuwaeleza ukweli wanachama wa tawi la Yanga lililopo Tandale linaloongozwa na mtu anayejiita Jitu, kwa lugha nyingine unaweza kusema ukimpiga teke chura unamsogeza mbele ya safari yake.

Tawi la Yanga Tandale ni moja kati ya matawi yenye hamasa kubwa kutokana na jitihada zao kuhamasisha kuingiza idadi kubwa ya wanachama pia wameonekana wana machungu na timu yao.

Lakini matamko yanayotolewa na tawi hilo kuhusu Yanga sidhani kama wanaitendea haki klabu yao ambayo msimu huu imekamata nafasi ya pili na kuvuliwa ubingwa wake iliokuwa ikiushikilia.

Kauli za viongozi wa tawi hilo zinaonyesha waziwazi kupingana na mwenyekiti wa Yanga bilionea Yusuf Manji, kumekuwa na uataratibu ndani ya tawi hilo kujifanya wasemaji kwenye masuala yanayoihusu Yanga wakati sivyo.


Kusajiliwa kwa wachezaji wawili Didier Kavumbagu na Frank Domayo na klabu ya Azam kumefanya wanachama hao kuulaumu uongozi wa Yanga hadi kufikia hatua ya kumdhalilisha mwenyekiti wao Manji.

Kusema kweli siwezi kukubaliana na hali hiyo inayoonyesha upotevu wa nidhamu ya hali ya juu, Manji na mwenyekiti wa Yanga aliyepo madarakani amefikia hatua ya kulifuta tawi hilo kwa mujibu wa sheria inayotokana na katiba ya Yanga.

Akiwa na mamlaka hayo ametangaza hadharani kulifuta tawi hilo, aidha kuwafuta wanachama sita, Waliofutwa uanachama ni Ally Kamtande, Isiaka Dude, Hamisi Matandula, Waziri Jitu Ramadhani, Mohamed Kigali Ndimba na Seleman Hassan Migali.

Kwa vyovyote waliofutwa wanatakiwa kuheshimu uongozi wao na si kuanza kulalamika kupitia vyombo vya habari, Kama alivyosema Manji Yanga haijakurupuka kuachana na Kavumbagu

isipokuwa waliomba mwongozo kutoka TFF kuhusu usajili wa wachezaji watano wa kigeni jambo ambalo hawakujibiwa.

Awali TFF ilitangaza kutumika kwa wachezaji watatu wa kigeni kuanzia msimu ujao lakini baadaye ikabadili agizo hilo na sasa ruksa klabu ya ligi kuu na daraja la kwanza kusajili wachezaji watano, aidha Manji alifafanua masuala kadhaa ikiwemo la kukataa kuongeza mkataba mwingine kwa Frank Domayo.

Wanayanga mnapaswa kutambua kuwa klabu yenu inaongozwa kwa mujibu wa sheria hivyo kila mmoja wenu anapaswa kuheshimu uongozi uliopo, Wana-Tandale wamekuwa katikamajibizano tangia uongozi wa Lyoid Nchunga na mpaka sasa wanaendelea na mambo hayo.

Umefika wakati kujirekebisha ama kuacha kabisa upotoshaji huo na kuutambua na kuuheshimu uongozi uliopo, Yanga ni moja hakupaswi kuwa na makundi wala mtengano wa ainha yoyote kwani hiki ni kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ambapo kila mwanachama anastahili kujitokeza na kuchukua fomu ya kuomba kuongoza.