KWA asilimia kubwa mnuso wa ubingwa wanukia Etihad baada ya Manchester City kuibuka na ushindi mtamu wa mabao 4-0 dhidi ya Aston Villa katika mchezo wa ligi kuu soka nchini England.
Ushindi huo umewarejesha Man City kileleni na sasa wanahitaji pointi moja tu kutwaa taji msimu huu.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa milango ya timu zote kuwa migumu.
Baada ya kuingia katika vyumba vya kuvalia nguo, Manuel Pellegrini aliwakumbusha vijana wake kuwa wamebakiwa na kazi ndogo kuchukua taji.
Man City waliporudi kipindi cha pili walikuja na kasi nzuri na katika dakika ya 64 na 72, Edin Dzeko alifunga mabao mawili.
Wakati Aston Villa wakitafuta njia ya kusawazisha, katika dakika ya 89, Stefan Jovetic aliifungia bao la tatu Man City.
Dakika ya 93, mwafrika mwenye kiwango cha juu zaidi, Yaya Toure alihitimisha karamu ya mabao na kuwafanya City wakaribie kuutwaa ubingwa wa pili ndani ya misimu mitatu.
City wameishusha Liverpool kileleni kwa kufikisha pointi 83, huku Liverpool wakibakia nafasi ya pili kwa poini 81. Timu zote zimecheza mechi 37.
Sare ya mabao 3-3 waliyopata Liverpool jumatatu ya wiki hii dhidi ya Crystal Palace imewafanya wawe katika wakati mgumu wa kufuta ukame wa miaka 24 bila kombe, na sasa wanawaombea dua mbaya Man City wafungwe mechi ya mwisho siku ya jumapili dhidi ya West Ham kwenye uwanja wa Etihad.
