WANASEMA msema kweli ni mpenzi wa mungu, tangia kuondoka kwa wachezaji wawili wa kutumainiwa katika klabu ya Yanga Mrundi Didier Kavumbagu na mzalendo Frank Domayo wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiushutumu uongozi wao.Wameenda mbali zaidi kwa kuitisha vikao vya mara kwa mara vikiwa na malengo ya kutaka kuwazuia wachezaji wengine wasiondoke huku shutuma nyingi zikielekezwa kwa viongozi kutokana na ukimya wao juu ya sakata hilo.
Wapo baadhi ya waliokuwa viongozi wa Yanga kipindi kilichopita wakisikika kuushutumu uongozi wa Yusuf Manji kuwa unaibomoa Yanga.
Kuchukuliwa kwa Kavumbagu na Domayo kunaonekana kumeiathili zaidi Yanga huku nyota hao kama roho ya Yanga, Lakini tukizama kiundani kuondoka kwa Kavumbagu na Domayo si pengo wala hakuna sababu ya kuushutumu uongozi.
Kwanza wachezaji wale hawakuuzwa na klabu moja kwa moja kiasi kwamba unaweza kuwashutumu kwa kujali maslahi kuliko umuhimu wa timu, wachezaji wale wameondoka kwa hiyali yao wenyewe kwani mikataba yao ilishamalizika.
Ni sawa na mpangaji katika nyumba ya kupanga akishamaliza mkataba wake si lazima kuendelea kuishi, anawezakutafuta nyumba nyingine ili mradi maisha yake yaendelee, uongozi wa Yanga hauwezi kushutumiwa kwa kuondoka nyota hao ambao mikataba yao ilishakwisha.
Mchezaji anapomaliza mkataba wake anakuwa huru, Kavumbagu alishamliza mkataba wake wa kuitumikia Yanga ambao ulikuwa wa miaka miwili, uongozi wa Yanga ulijitahidi kuongea naye ili waongeze mkataba mwingine mchezaji huyo alikimbilia kwenye vyombo vya habari na kutangaza kuwa Yanga imemsusa wakati si kweli.Haikuchukua siku Azam fc mabingwa wa soka Tanzania bara wakatangaza kumchukua, uongozi wa Yanga hauwezi kuingia kwenye shutuma ya aina yoyote hapo, siku moja baadaye kiungo wa kutegemewa na Yanga pamoja na timu ya taifa, Taifa Stars Frank Domayo naye alisaini Azam miaka miwili.
Kama ilivyokuwa kwa Kavumbagu, Domayo alimaliza mkataba wake wa kuitumikia Yanga, uongozi wa Yanga ulifanya naye mazungumzo ya kurefusha mkataba wake tangia mwezi septemba mwaka jana lakini Domayo alikuwa akiupiga danadana.
Mara kwa mara Domayo alisingizia mjomba wake ambaye ndiyo wakala wake, alikuwa akisema mpaka awepo mjomba wake ili aweze kusaini, siku zilizidi kwenda hadi mwisho mwa msimu ahadi za kuwasili mjomba wake zilizidi kuwa agenda katika kinywa cha Domayo.
Mara tukasikia amesaini Azam miaka miwili, uongozi wa Yanga hauwezi kuingia hatiani kwa hilo, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga mfike wakati kuheshimu kauli zinazotolewa na viongozi wenu wa Yanga na kuelewa mikakati ya jumla ya klabu yenu muipendayo.
Vile vile mnapaswa kujua uwezo wa wachezaji wote wa Yanga na umuhimu wa wachezaji kwa ujumla na kila mmoja alifanya kitu gani ambacho kitabakia kama kumbukumbu ndani ya Yanga, kama mnakumbuka vizuri Didier Kavumbagu alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotaka kutemwa katika kikosi hicho.
Kavumbagu alishindwa kuisaidia Yanga katika michuano mbalimbali ikiwemo ligi kuu, kushuka kwake kiwango kulipelekea kuingia kwenye vita ya maneno ya mchezaji mwenzie Jerry Tegete.
Vita hiyo ya maneno ilishamili hasa baada ya Tegete kuonyesha ustadi mkubwa wa kupachika magoli, Kavumbagu alikuwa gumzo kqwenye vyombo vya habari akilalamika kuwa anarogwa na Tegete.Kwa utashi wangu siwezi kuamini masuala ya ushirikina kwenye soka ingawa nasikia upo, Kavumbagu alipotea kwenye mstari baada ya kuzidiwa na Tegete, hata sasa ukitazama kiundani Tegete ameonyesha makali kuliko Kavumbagu isipokuwa majeruhi yalimtesa benchi.
Tegete amecheza mechi saba amefunga magoli sita uoni tofauti hapo na Kavumbagu alicheza mechi zote za ligi lakini amefunga magoli saba tu, tofauti ipo kubwa tena sana isipokuwa alionyesha umakini mkubwa anapolisogelea goli kiasi kwamba mabeki wa timu pinzani wametumia mbinu mbadala ya kumkaba wawili wawili.
Kiwango cha Kavumbagu kilinusuriwa na mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa mwaka jana ambapo Yanga ilishinda 2-0, katika mechi hiyo Kavumbagu alifunga goli la kwanza kabla ya Hamis Kiiza kufunga la pili.
Kuondoka kwa Kavumbagu Yanga kusiwe chanzoi cha kuleta mfarakano wakati mchezaji mwenyewe amejikuta anacheza peke yake pasipo ushindani wowote kutoka kwa straika mwingine ndani ya Yanga.Tegete amekuwa majeruhi mara kwa mara lakini kiuwezo Tegete anabaki kuwa juu, amecheza mechi saba amefunga magoli sita, wakati Kavumbagu amecheza mechi zote amefunga goli saba.Kuhusu Frank Domayo sina mengi ya kumwelezea kwakuwa kiwango chake kipo juu na amekuwa tegemeo kwenye timu ya taifa, lakini Domayo ameanza kuchukua nafasi ndani ya Yanga baada ya kiungo mwingine wa timu hiyo Salum Telela kuumia.
Ikumbukwe Telela ndiye kiboko ya Azam fc ambapo goli lake bado lina kumbukumbu nzito ambapo Yanga iliifunga Azam katika mechi maalum ya kugombania Ngao ya Hisani, mechi hiyo ilichezwa mwaka jana ambapo Azam ilitoka kuweka kambi nchini Afrika Kusini lakini ikakubali kichapo cha 1-0.
Tangia kuumia kwa Telela Yanga ilianza kumtumia Domayo kama mchezaji wa kudumu katika nafasi hiyo, hadi sasa Telela anauguza majeraha benchi na Domayo akawa katika kikosi cha kwanza.
Utagundua nyota wote hao wawili Domayo na Kavumbagu wamepata nafasi Yanga kutokana na wenye namba zao kuwa majeruhi ambao ni Tegete na Telela, kuondoka kwao kusiwe matatizo ndani ya Yanga kwani bado Yanga inao nyota wengine wenye uwezo mkubwa kama iliokuwa nao Kavumbagu na Domayo.
Salum Telela ambaye ndiye mwenye mchango mkubwa ndani ya Yanga kwani ameweza kuleta ngao ya hisani kwa kufunga goli zuri dhidi ya Azam fc, historia bado inawasuta Kavumbagu na Domayo kwani licha ya uwepo wao katika kikosi cha Yanga bado hawajaweza kuzifunga Simba na Azam katika ligi iliyomalizika ya msimu wa 2013/14.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0755 522216