Nyota huyo wa zamani amefanyiwa upasuaji huo kwa
gharama za serikali baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Michezo, Leonard Thadeo kufika nyumbani kwa mchezaji huyo.
Hatua hiyo ya serikali imechangiwa na mfululizo wa
makala zilizoandikwa katika safu ya Mkongwe kwenye gazeti hili makala
iliyoelezea maisha duni na maradhi ya kiharusi yaliyosababisha kupooza
mkono na mguu wa kushoto wa mchezaji huyo.
Habari za nyota huyo zilisababisha Mbunge wa
Kinondoni, Iddi Azzan kuhoji iwapo serikali ina mpango wowote wa
kuwasaidia mashujaa wa zamani katika michezo akiwamo Mtagwa, mchezaji
pekee nchini ambaye picha yake ilitumika katika stempu zilizochapishwa
mwaka 1982.
Thadeo alikiri kufika nyumbani kwa Mtagwa kumjulia
hali lakini alikataa kuzungumzia kwa undani kwa madai kuwa suala la
nyota huyo lilishatolewa ufafanuzi na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni
na Michezo wakati wa kuhitimisha bajeti ya wizara hiyo hivi karibuni
katika vikao vya Bunge.
Akizungumza nyumbani kwake jana Jumatatu, Mtagwa
alisema kuwa alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan baada ya
kufuatwa na viongozi wa idara ya michezo.
“Alikuja Thadeo kuiwakilisha serikali na
waliwezesha kufanyiwa upasuaji na Jumatano (kesho) naenda kutoa nyuzi,”
alisema Mtagwa na kuongeza kuwa upasuaji huo umefanikiwa baada ya
madaktari kumpima na kuthibitisha kuwa kiwango cha msukumo wa damu
kimeshuka.
Mtagwa alisema licha ya ukosefu wa fedha
uliosababisha ashindwe kufanyiwa upasuaji mapema lakini pia kiwango
chake cha msukumo wa damu kilichosababisha apooze mkono wa kushoto na
mguu mara nyingi ilikuwa juu hivyo kuwafanya madaktari kuahirisha
upasuaji huo mara kwa mara.
“Kuna wakati kabla serikali haijajitokeza kuna
watu walitaka kunisaidia lakini presha ilikuwa tatizo,” alisema na
kuongeza kuwa anaendelea vizuri baada ya upasuaji na anaamini kuwa
akiendelea kupata matibabu stahiki afya yake itaimarika.