Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuifunga Azam 2-0 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa mwaka jana.
Akizungumza na mtandao huu jana, Kaimu katibu Mkuu wa Yanga Lawrance Mwalusako alisema "wachezaji ambao walikuwa wameenda kusalimia makwao hasa wale wa nje ya Dar es Salaam wameanza kurejea.
"Mpaka kufikia kesho (leo) wachezaji wote watakuwa wapo hapa (hivyo) Jumatatu mazoezi na maandalizi kwa ajili ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati yataanza."
Yanga itaanza rasmi mazoezi chini ya kocha wake Ernest Brandts atakayewasili nchini kesho kutokea Uholanzi alipokuwa ameenda kwa ajili ya mapumziko mafupi tangu kumalizika kwa ligi kuu ya Bara wiki mbili zilizopita.
Mashindano hayo ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati yatafanyika mwezi ujao nchini Sudan.
Lengo la kocha huyo ni kuhakikisha timu inatetea ubingwa wake ambao ulichukuliwa na Yanga wakati kikosi hicho kikifundishwa na Tom Santifiet, alisema Mwalusako.
Santifiet alitimuliwa baada ya mechi mbili za kwanza za msimu.
Mazoezi ya Yanga yataanaza huku ikiwakosa wachezaji wake nyota sita waliomo kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' na Haruna Niyonzima ambaye ameitwa kwenye timu ya taifa ya Rwanda.
Wachezaji wa Yanga waliopo Stars ni Ally Mustapha 'Bartez', Athuman Iddi 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Canavaro', bila kumhesabu Mrisho Ngasa waliyemnyakua mdomoni mwa Simba aliyokuwa akiichezea kwa mkopo.