Straika wa Yanga, Kpah Sherman, raia wa Liberia, amefunguka kuwa anahitaji kuwa mchezaji bora katika kikosi cha timu hiyo kwa kukisaidia kwenye ligi na michuano ya Kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Sherman amesajiliwa Yanga katika usajili wa dirisha dogo na tangu atue Jangwani kiwango chake kimekuwa kikiwakuna mashabiki.
Sherman ameeleza kuwa, anajua Yanga wamemuamini ndiyo maana wamemsajili, hivyo kama mchezaji wa kulipwa, anahitaji kuitumikia ipasavyo timu yake hiyo ili iweze kufanya vizuri katika ligi na michuano ya kimataifa.
“Mimi ni mchezaji professional na ninatambua miiko ya mchezaji wa kulipwa, Yanga imeniamini na imenisajili, hivyo nahitaji kuitumikia kwa nguvu kuhakikisha inafanya vyema kwenye ligi na michuano ya kimataifa.
“Nitajitahidi kuhakikisha najaribu kuwa bora katika timu yangu kwa kufanya vyema kwa kujituma uwanjani na sihofii ushindani wa namba,” alisema Sherman.