Albert Mangwea
MWILI wa mwanamuziki mahiri wa kizazi kipya, Albert Mangwea aliyefariki nchini Afrika Kusini katikati ya wiki, unatarajiwa kuagwa kwenye viwanja vya Leaders Club keshokutwa Jumatatu.
Viwanja vya Leaders Club ndipo mahali ambapo mwili wa mcheza filamu maarufu Afrika wa Bongo movie, Steven Kanumba, aliyefariki zaidi kidogo ya mwaka mwaka mmoja uliopita uliagwa pia mapema mwaka jana.
Aidha, mwili wa 'Ngweair' uliokuwa urudishwe leo mchana, utaletwa kesho kwa kuwa utalazimika kuchelewa kutokana na kuwapo kwa shughuli nyingine ya kuuaga nchini humo.
Kwa mujibu wa Msemaji wa kamati ya mazishi ya msanii huyo, Adam Juma, waombolezaji wa Afrika Kusini watauaga mwili huo leo na kesho utawasili nchini saa nane mchana.
Mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege, mwili huo utapelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuifadhiwa kusubiri taratibu nyingine katika ratiba ya mazishi ya 'Ngweair'.
"Baada ya kuagwa Jumatatu kwenye viwanja vya Leaders, mwili wa ndugu yetu utapelekwa nyumbani kwa mama yake mzazi Kihonda mjini Morogoro ambapo huko nako ndugu jamaa na marafiki watapata nafasi ya kuuaga na tunategemea maziko yatafanyika siku ya Jumanne," alisema Juma.
Akiojiwa kwenye kituo kimoja cha Radio mapema jana asubuhi, Kaka wa marehemu Kennedy Mangwea, alisema familia yao imemteu Millard Ayo kuiwakilisha nchini humo na kusimamia taratibu za kuuleta mwili wa 'Ngweair' nchini.
Marehemu alitamba na nyimbo mbalimbali wakati wa uhai wake, na alifariki dunia ghafla Jumatano.
Baadhi ya nyimbo zake zilizotamba ni pamoja na 'Mikasi', '(Nakesha kama) CNN', Nipe Dili (nikamate mahela)', 'Ghetto Langu' na 'She Got a Gwan'.
Nyingine ni 'Ndani ya Club, 'Spidi 120' na 'Mtoto wa Jah Kaya' ambayo iliwahi kusema ilitasfiriwa visivyo kuwa ni ya kumpigia debe mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete.
Albamu yake mwisho ni 'A.k.a Mimi' na pia alishirikiana kwa mafanikio katika uimbaji na wasanii mbalimbal wakali wakiwemo Lady Jay Dee na Mwana FA.